CURRENT NEWS

Wednesday, January 3, 2018

TANESCO TABATA WALALAMIKIWA KUTELEKEZA NYAYA, NGUZO ZA MRADI KIFURU, KINYEREZI

Magari na pikipiki zikipita kwa shida Mtaa wa Tanganyika, Kifuru Kata ya Kinyerezi jijini Dar es Salaam, eneo ambalo nyaya na nguzo za mradi wa umeme unaodaiwa kutelekezwa na TANESCO kituo cha Tabata kwa muda sasa baada ya kuangushwa na mvua za mwishoni mwa mwaka 2017. Magari na pikipiki zikipita kwa shida Mtaa wa Tanganyika, Kifuru Kata ya Kinyerezi jijini Dar es Salaam, eneo ambalo nyaya na nguzo za mradi wa umeme unaodaiwa kutelekezwa na TANESCO kituo cha Tabata kwa muda sasa baada ya kuangushwa na mvua za mwishoni mwa mwaka 2017.

  WAKAZI wa Kata ya Kinyerezi eneo la Kifuru kwa Kinana wameulalamikia uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kituo cha Tabata jijini Dar es Salaam kwa kitendo cha kutelekeza nguzo na nyaya za mradi wa umeme eneo hilo ambapo zime geuka kero.

 Wakizungumza jana eneo hilo kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi wakazi hao, wamesema TANESCO kituo cha Tabata walileta nguzo na nyaya tangu mwaka jana na kuziweka barabara inayoelekea King'azi (Kwa Godoro) Mtaa wa Tanganyika ambapo baada ya mvua za mwishoni mwa mwaka jana 2017 baadhi ya nguzo zilianguka na nyaya kutandaa chini jambo ambalo limekuwa kero baada ya kuziba barabara ya mtaa huo na magari kupita kwa taabu.

 Mkazi wa Mtaa wa Tanganyika, Rashid Abdallah alisema mradi huo umechukua zaidi ya miaka miwili sasa huku wateja walioomba umeme eneo hilo wamekuwa wakizungushwa kwamba wasubiri mradi huo bila ya mafanikio.

 "...Tumeomba umeme muda mrefu sana tunaambiwa kusubiri mradi lakini mradi ndio kama hivyo wamekuja wamefunga nyaya baada ya mvua kunyesha zimeanguka na wamezitelekeza hapo hapo chini...tunapita kwa shida na wengine kwa hofu maana nyaya za umeme zipo chini kabisa si wote wapita njia hazijafungwa umeme sasa hii ni hatari," alisema

Mkazi huyo wa Mtaa wa Tanganyika. Alisema kwa sasa wamekuwa kama walinzi wa nguzo na nyaya hizo za TANESCO mtaani hapo maana wanahofia zikiibiwa huenda matumaini ya mradi huo wanaoahidiwa kila kukicha kukamilika ukatoweka kabisa.

"Sasa hivi tumegeuka walinzi maana tunajitahidi haya manyaya yao (waya za TANESCO) waliotelekeza hapo chini baada ya kuanguka yasiibiwe...," alisema Abdallah.   Sehemu nyingine katika mtaa huo nyaya zimelala chini pamoja na nguzo kupinda. Sehemu nyingine katika mtaa huo nyaya zimelala chini pamoja na nguzo kupinda. Baadhi ya nguzo na nyaya za TANESCO Kituo cha Tabata Dar es Salaam zinazodaiwa kutelekezwa na kituo hicho kwa muda sasa baada ya kung'olewa na mvua. Wakazi wa eneo hilo wameilalamikia TANESCO kwa kushindwa kutatua kero hiyo na kukamilisha mradi.

 Kwa upande wake mkazi mwingine wa eneo hilo, Senzekwa Magila alisema wanashangaa kuzungushwa maombi yao ya kufungiwa umeme wakielezwa kusubiri mradi ambao haukamiliki ilhali wanaendelea kutaabika.

Alisema TANESCO inapaswa kujifunza na kuwa makini kwa uongozi wa sasa kwani unahimiza uchapaji kazi bora unaolenga kuiingizia Serikali na taasisi zake mapato ya kutosha, jambo ambalo wanashangaa wateja wanaomba huduma zaidi ya miaka miwili bila mafanikio.

 "..Tunashangaa sana wateja tunaomba umeme ili tuweze kuchangia kipato cha shirika na hatimaye Serikali lakini hadi leo tunazungushwa, lakini mapato yetu eneo hili yangeweza kuchangia pato la TANESCO na Serikali. Sasa hivi tunajadiliana kwenda kuwaona viongozi gazi za juu watusaidie labda huenda tutafanikiw," alisema mkazi huyo.

 Naye mkazi mwingine ambaye alikataa kutaja jina lake alisema kinachowakaza zaidi ni kitendo cha maeneo yote yaliozunguka mtaa huo kuunganishwa umeme lakini wao Mtaa wa Tanganyika hadi leo wamekuwa wakipigwa danadana bila mafanikio.

 Alisema wengi wao wamejinyima na kuanza kufunga mfumo wa umeme mapema katika nyumba zao lakini hadi leo hawajaunganishwa.

"Ukienda kutaka kulipia wanakwambia subiri umeme wa mradi sasa huu umeme wa mradi unatoka nje ya nchi au hapa hapa Tanzania...maana hatuelewi. Mi nadhani kama wameshindwa kutuunganisha waje waondoe kero zao hapa mtaani kwetu maana umeme hatuna lakini kila kukicha tunalinda waya zao na nguzo walizozitelekeza na kuziba njia hapa," alisema mkazi huyo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania