CURRENT NEWS

Sunday, January 7, 2018

UMISSETA, UMITASHUMTA KUJA KIVINGINE

  
 Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Elimu anayeshughulikia Sekondari, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Paulina Mkwama, akifafanua jambo kwa wajumbe wakati wa kikao na Wadau wa Michezo ya Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) mjini Dodoma. Kushoto kwake ni Mohemed Kiganja, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT)
Mohemed Kiganja, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi cha siku mbili mjini Dodoma kuhusu Michezo ya Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA), kulia kwake ni Mkurugenzi wa Michezo toka Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Yusuph Singo

Mratibu wa Michezo Ofisi ya Rais TAMISEMI, Salum Mkuya akitoa mapendekezo ya kuanzisha soka la wanawake na kurudisha michezo mingine kama ngoma kwa msisitizo ili vijana wajenge uzalendo.

Mohemed Kiganja, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) akitoa ufafanuzi wa baadhi ya taratibu za michezo na kanuni za UMISSETA na UMITASHUMTA
    ........................................................

Na. Fred J. Kibano
Mashindano ya michezo kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) yameanza kufanyika baada ya kufanyika kwa tathmini ya mashindano hayo ya mwaka jana, 2017 ambapo baadhi ya michezo itaongezwa.
Akifungua kikao kazi cha siku mbili mjini Dodoma, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Elimu anayeshughulikia Sekondari, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Paulina Mkwama, amesema kikao hicho nyeti kimewakutanisha wajumbe toka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wadau wengine wakiwemo Maafisa Michezo toka Mikoa na Halmashauri, Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri na Baraza la Michezo la Tanzania ili kufanya tathmini na kuanza maandalizi ya michezo hiyo Juni, mwaka 2018.
“Kimsingi Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo pamoja na Wadau wengine wamekutana kwa ajili ya kufanya tathmini ya mashindano ya UMITASHUMTA (Michezo kwa Shule za Msingi Tanzania) na ile ya shule za sekondari (UMISSETA), yaliyofanyika mwaka jana (2017), na kuweka mikakati ya namna bora ya kuendesha michezo kwa mwaka 2018, ndio lengo kuu la kikao hiki”
Bi. Mkwama amesema, baada ya kikao hicho, kitawezesha kupata mikakati madhubuti kwa mashindano mapya hasa baada ya kupitia taarifa za michezo iliyofanyika mwaka uliopita, 2017 ili kuweka mikakati mizuri itakayoboresha michezo hiyo ambayo ndiyo muhimili wa wachezaji wote wa Taifa hili.
Aidha, amesema watapitia bajeti ya michezo ya mwaka 2017 na kuona changamoto zilizotokea ili kuzikabili kwa michezo ya mwaka huu, 2018 ikiwa ni pamoja na kushirikisha Wadau ambao wataiunga mkono Serikali hususani katika bajeti na vifaa.
Pia Miongozo yote ya michezo itapitiwa ili kujua changamoto zote lengo likiwa ni kuboresha michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA nchini ambayo pia hukuza taaluma mashuleni. 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Mohamed Kiganja, amewataka Maafisa Michezo kuteua Walimu ambao wanauelewa wa michezo na ifanyike mapema ili kuondoa kasoro zilizo jitokeza michezoni mwaka 2017.
Naye Mratibu wa Michezo Ofisi ya Rais TAMISEMI, Salum Mkuya, amesema watatoa mapendekezo kwa baadhi ya michezo iongezwe kama vile soka la wanawake ambalo Tanzania inafanya vizuri ikiwa ni nchi tano tu kwa bara zima la Afrika, lakini pia ngoma kwani michezo inasaidia sana vijana kujenga uzalendo kwa nchi yao.
Michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA hufanyika kila mwaka kwa kukutanisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini na kwa mwaka huu matarajio ni kuwahusisha wanafunzi wasiopungua 6,480 wa shule za msingi na sekondari. Changamoto zilizojadiliwa ni pamoja na wanafunzi wenye mahitaji maalum, vigezo vya umri, vifaa, bajeti ya usafiri na chakula na mengineyo ambayo yatafanyiwa kazi kimkakati. 

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania