CURRENT NEWS

Tuesday, January 30, 2018

WANANCHI MIL.25 BADO HAWAFIKIWI NA HUDUMA ZA MAHAKAMA-JAJI MKUU

 Jaji mkuu, prof.Ibrahim Juma (wa kulia pichani)akifurahi baada ya kuzindua mahakama ya wilaya ya Bagamoyo ambayo imejengwa kwa gharama ya mil.519.3 ,ikiwa ni sehemu ya ujenzi pia wa nyumba mbili za mahakimu ,ambazo zimegharimu mil.109 ,pichani kushoto ni mkuu wa Mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo.(picha na Mwamvua Mwinyi)

Jaji mkuu, prof.Ibrahim Juma (wa pili kutoka mbele)akitembelea nyumba mbili za mahakimu ,zilizojengwa kwa gharama nafuu ya sh.mil.109,mara baada ya kuzindua mahakama ya wilaya ya Bagamoyo ambayo imejengwa kwa gharama ya mil.519.3 ,wa tatu kutoka mbele ni mkuu wa Mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo.(picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo

ZAIDI ya wananchi milioni 25 ,bado hawafikiwi na huduma za mahakama katika ngazi mbalimbali kutokana na tatizo la upungufu wa majengo ya kisasa ya mahakama za wilaya na za hakimu mkazi nchini .

Takwimu hiyo imebainika baada ya kukusanywa kwa ajili ya mpango mkakati wa mahakama ,huduma za mahakama za mahakama za ngazi mbalimbali .

Kutokana na changamoto hiyo ,serikali imeendelea kuongeza nguvu katika maboresho ya mahakama zake kwa lengo la kuongeza idadi ya wananchi watakaopata huduma za kimahakama.

Hayo yalisemwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof.Ibrahim Juma ,wakati alipokuwa akizindua mahakama ya kisasa ya wilaya ya Bagamoyo ,mkoani Pwani .

Alisema upatikanaji na utoaji haki kwa wakati na kwa kuzingatia maadili ndio kile wananchi wa Tanzania wanachotaka kuona kutoka ngazi zote za mahakama.

"Ili kufikia wajibu huu wa kikatiba ,mpango mkakati wa mahakama umebaini kuwa wananchi wanategemea kuona mahakama inaendeshwa kwa misingi ya utawala bora,uwajibikaji na usimamizi bora wa raslimali " alisema Jaji mkuu .

Pamoja na hayo ,Prof.Ibrahim alisema mpango mkakati unaitaka mahakama kuimarisha imani ya wananchi kwa mahakama hizo na kuwashirikisha wadau kwenye maboresho ya mahakama.

Jaji mkuu ,alieleza wakati wilaya ya Bagamoyo inaposheherekea kuwa na jengo jipya, lakini bado ina changamoto ya mahitaji makubwa ya majengo ya mahakama za mwanzo angalau katika kila Tarafa.

Prof.Ibrahim alisema ,wilaya hiyo ina kata 26 na mahakama za mwanzo saba pekee hivyo inahitaji majengo hayo zaidi ambayo ndio hubeba mzigo mkubwa wa mashauri.

Hata hivyo, alisema haitoshi kupata jengo la kisasa lenye vifaa vya TEHAMA bila kutatua changamoto zinazozuia upatikanaji wa haki kwa wakati na yenye maadili .

"Itashangaza mahakama ya wilaya kama hii imewekewa mifumo hiyo lakini unapofika unakuta bado matumizi ni yaleyale ya kizamani na ya karne iliyopita" alisema Jaji mkuu.

Prof. Ibrahim alisema mwaka huu ,katika wiki ya sheria imesisitiza umuhimu wa kuondoa changamoto mbalimbali ikiwemo matumizi ya Tehama katika mahakama.

Pia kutoa elimu kwa wananchi waelimishwe kuhusu dhana ya usuluhishi kwa kumaliza mgogoro kabla ya kuipeleka migogoro hiyo mahakamani.

Jaji mkuu, aliwataka watumishi wa mahakama hiyo, kuwatumikia wananchi na kuwatendea haki pasipo kugeuza jengo  hilo soko la rushwa na ukiukwaji wa maadili .

Nae, Jaji Kiongozi Fredrick Wambali alisema Bagamoyo ilikuwa ikisubiri jengo la aina hiyo kwa mwaka wa 92 sasa .

Wambali alisema, wataendelea kusimamia jengo hilo jipya na maadili .

Kwa upande wake ,mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo ,alieleza wilaya ya Rufiji na Kibiti zinakabiliwa na changamoto ya majengo chakavu .

Aliomba wilaya hizo kupatiwa majengo ya mahakama ili kufikisha huduma stahiki katika jamii.

Ndikilo ,alitaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya watu kuhodhi ardhi ama kuvamia maeneo nankujihalalisha kukimbilia mahakamani suala linalokwamisha uwekezaji .

Aliomba mashauri ya kesi za mimba za utotoni na migogoro ya wakulima na wafugaji iongezwe kasi ili kuleta matumaini kwa wananchi wa pande zote mbili mlalamikiwa na mlalamikaji.

Awali mkurugenzi msaidizi ,mipango na bajeti mahakama ya Tanzania ,Erasmus Uisso alisema, jengo hilo limegharimu kiasi cha sh. mil.519.8 ambalo pia linahusisha nyumba mbili za mahakimu zilizotumia sh.mil.109.5. 

Alisema jengo hilo la mahakama ya wilaya ya Bagamoyo ,ina ukumbi mkubwa ,ofisi na mahabusu ya wanawake,watoto na wanaume .

Uisso alisema ,sehemu ya uzinduzi huo ni mwendelezo wa kuzindua mahakama nyingine sita katika wiki hii ya sheria ikiwemo Mkuranga,Kigamboni,Ilala,mahakama ya mwanzo Kawe ,mkoa na wilaya ya Kibaha ambayo imezinduliwa mwaka uliopita .

Kwasasa wanaendelea kujenga mahakama nyingine tano za mikoa na 11 za wilaya nchini.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania