CURRENT NEWS

Saturday, January 6, 2018

WANANCHI WA MBUCHI-MBWERA KUPATA DARAJA LA KUDUMU

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo(katikati) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Eng.Evarist Ndikilo na viongozi wengine wa Mkoa huo wakati wa ziara yake ya kuweka jiwe la msingi katika Daraja la Mbuchi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akimpa MKandarasi maelekezo juu ya umuhimu wa daraja la Mbuchi kukamilika kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu kutokana na hali adha wanayoipata wananchi wa maeneo hayo kwa hivi sasa.


 Hawa ni wananchi wa kijiji cha Mbwera wakivuka kwa kutumia Mtumbwi kuja kijiji cha Mbuchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali hii ni kutokana na kukosekana kwa daraja linalounganisha vijiji hivyo lakini kwa sasa Ujenzi wa daraja hilo umeanza na utakamilika baada ya mwaka mmoja.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akimskiliza Meneja wa Tarura Wilaya ya Kibiti kuhusu maendeleo ya Ujenzi wa Daraja la Mbuchi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akizungumza na wananchi wa vijiji vya Mbuchi na Mbwera kwenye Mkutano wa hadhara wakati alipokuwa anaweka Jiwe la Msingi kwenye ujenzi wa Daraja la Mbuchi.
         ..........................................................................................................

Nteghenjwa Hosseah,Kibiti.

Wananchi wa Kata ya Mbuchi na Mbwera Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, kwa kipindi kirefu wamekuwa wakitaabika kutokana na ukosefu wa Daraja linalounganisha wananchi wa vijiji hivyo vyenye wakazi zaidi ya 24,000.

Kukosekana kwa Daraja hilo kumesababishwa kuongezeka kwa gharama za maisha kwa wananchi wa Mbuchi na Mbwera huku akina mama wanaojifungua na wagonjwa wakishindwa kufikishwa kwenye maeneo ya kutolea huduma za matibabu kwa urahisi.

Vijiji hivyo  vimetengenishwa na Mto Mberambe ambao ni Tawi la Mto Rufiji na kutengeneza Delta ya Kaskazini tangu kuanzishwa kwake havijawahi kuwa na Daraja la kuwaunganisha katika shughuli zao za kila siku za kujiletea Maendeleo.

Kufuatia hali hiyo, Wananchi wa maeneo haya wamekuwa wakitumia Mitumbwi kuwavusha kutoka eneo moja hadi jingine ambapo hutozwa Tsh 200 kwa safari moja na Pikipiki kutozwa Tsh 1000 kwa safari na huduma  hiyo ya usafiri imekuwa ikipatikana kuanzia saa kumi na mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni.

Akizungumza na wananchi alipotembelea eneo hilo miezi kadhaa iliyopita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo alijionea adha hiyo na kuwaagiza Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini(Tarura) kuchukua hatua za haraka kwa kujenga Daraja la kudumu litakalounganisha wananchi hao wa maeneo hayo.

Kufuatia maagizo hayo, Leo Januari 05,mwaka huu, Waziri Jafo ametembelea katika vijiji hivyo kukagua Ujenzi wa Daraja hilo na kuweka jiwe la Msingi katika ujenzi huo.

Akikagua daraja hilo, Waziri Jafo amesema alitegemea kuona Mkandarasi amepiga hatua  kwenye ujenzi huo lakini utendaji wake unaenda taratibu licha ya mkandarasi huyo kudai kuwa amechukua muda mrefu kutokana na ubovu wa barabara hivyo ilikuwa ni vigumu kufikisha vifaa vya ujenzi.

“Nimepita katika barabara hii na nimeona Ubovu wake lakini haya yote ulitakiwa uyafahamu tangu mwanzo wakati unaomba kazi hii, sasa mpaka leo hakuna kazi ya maaa iliyofanyika hapa kama unahisi huwezi bora useme mapema ili tutafute Mkandarasi mwingine mwenye uwezo mkubwa” amesema Jafo.

Ameongeza kuwa wananchi hao wamepata tabu kwa kipindi kirefu, wameteseka sana,wamenyanyasika hivyo hawezi kuvumilia kuona hali hiyo inaendelea kwa kuwa wananchi hao ni sawa na wananchi wengine na wanahitaji huduma muhimu kama Daraja hilo liweze kuwaunganisha.

" Katika hili Mkandarasi utaniona mbaya na nitakuwa narudi mara kwa mara kukagua maendeleo ya ujenzi wa hili daraja,"amesema 

Awali akieleza maendeleo ya Ujenzi huo, Meneja wa Tarura Wilaya ya Kibiti  amesema ulianza machi mwaka ,2017 lakini kutokana na mvua zilizokuwa zinaendelea kunyesha iliyosababisha Mkandarasi kushindwa kupeleka vifaa kwenye eneo la kazi na kuomba wapitie Mkataba na baada ya kufanya hivyo kazi ilianza rasmi mwezi Septemba,2017 na itachukua miezi 15 kukamilika.

Daraja hilo ambalo litabadilisha maisha ya wananchi wa Mbuchi-Mbwera  na linatarajiwa kugharimu Tsh Bilioni 2.4 na litakamilika mwezi Novemba 2018.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania