CURRENT NEWS

Tuesday, February 6, 2018

CCM BAGAMOYO IMEUFUTA WARAKA UNAOWAKATAZA WASIHOJI WATENDAJI WA SERIKALI

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)wilayani Bagamoyo,alhaj Abdul Sharif ,akizungumza na wanachama wa chama hicho na baadhi ya wananchi (hawapo pichani) huko kata ya Miono wilaya Bagamoyo.(picha na Mwamvua Mwinyi)


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)wilayani Bagamoyo,alhaj Abdul Sharif ,(wa katikati aliyevaa shati lenye rangi ya kijani)alipopokelewa na baadhi ya wanachama wa chama hicho huko kata ya Miono ,wilaya Bagamoyo.(picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo,alhaj Abdul Sharifu amefuta waraka uliotolewa wilayani hapo, ambao unakataza viongozi wa chama kutokuwa na fursa ya kuwahoji watendaji wa serikali.      
Aliyasema hayo baada ya kufanyika sherehe za miaka 41 ya CCM katika kata za Mbwewe, Miono na Lugoba .
Alhaj Sharifu alisema waraka huo unasababisha baadhi ya watendaji kutowajibika ipasavyo kwa wananchi.
Alielezea waraka huo unaonekana una maslahi ya watu binafsi ambao unakwenda kinyume na maslahi ya wananchi hivyo hauna manufaa yoyote zaidi ya kuwakandamiza wananchi.
“Naufuta maana haiwezekani watendaji wa serikali waachwe wafanye wanavyotaka hata wakiharibu tusiwahoji ,wakati chama kina wajibu wa watendaji wa serikali ,” alisema Sharifu.
Aidha Sharifu alisema,baadhi ya mambo yamekuwa hayaendi kutokana na watendaji hao kujisahau na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwani hakuna watu wa kuwahoji.
“Kila siku Rais anasisitiza chama ndiyo kimeunda serikali hivyo watendaji wake lazima wasimamiwe na chama ,hatuwezi kuona mambo yanaharibika halafu tukae kimya ikifika nyakati za uchaguzi tunaonekana hatujafanya lolote,Hili halikubaliki,” alisema Sharifu.
Alisema ilani inayotekelezwa ni ya CCM hivyo lazima viongozi wa CCM wasimamie watendaji na hata ikiwezekana kuwaondoa wale ambao wanashindwa kuwajibika kwenye nafasi zao.
Nae mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Abubakary Mlawa alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha miradi mbalimbali ya maenedeleo ya wananchi inakamilika kwa muda uliopangwa.
Mlawa alisema kuwa jumuiya zote za chama zimeungana kuhakikisha zinawatumikia wananchi kwa kuhamasisha masuala ya maendeleo na kuibua miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na elimu, afya, maji, barabara, kilimo na mifugo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania