CURRENT NEWS

Thursday, February 1, 2018

DC MTATURU AFANYA MAZUNGUMZO NA UONGOZI WA CWT WILAYA.


Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mheshimiwa Miraji Mtaturu kulia kwake akiwa na mwenyekiti wa CWT wilaya mwalimu Ladislaus Nkuu,katibu tawala wa wilaya hiyo  Winfrida Funto na kushoto kwake ni katibu wa CWT mwalimu Isdori Ndarabe na mwenyekiti wa halmashauri Ally Mwanga.
............................................................
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida mheshimiwa Miraji Mtaturu  amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa chama cha walimu(CWT)wilayani humo na kuwahakikishia kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya mheshimiwa Rais Dokta John Magufuli imedhamiria kuondoa changamoto zinazowakabili ikiwemo madeni ya walimu.

Mheshimiwa Mtaturu ameeleza  hayo  baada ya viongozi hao kwenda kumtembelea ofisini kwake.
Amesema serikali inatambua changamoto hizo na imedhamiria kwa dhati kuziondoa ndani ya muda mfupi.

“Mi nawaomba niwatoe hofu,chini ya Rais wetu mheshimiwa  Magufuli changamoto zenu zinazowakabili ikiwemo madeni ya walimu zitatatuliwa,”alisema Mtaturu.

Amewaahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuzibaini na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu ndani ya wilaya ili kuongeza ari ya walimu kufanya kazi na hatimaye ufaulu uongezeke kwa wanafunzi.

"Changamoto nyingine zimetokana  na fursa ya serikali kutoa elimu bure ambapo uandikishaji wa wanafunzi unaongezeka kila mwaka hivyo kama  serikali  tutaendelea kuzitatua kwa kushirikiana na wadau wote wa elimu na kwa kuanzia tumeanzisha mfuko wa elimu ambao utasaidia kwa namna moja ama nyingine kutatua baadhi ya changamoto wilayani kwetu,"alisema mkuu wa wilaya huyo.

Kwa upande wake katibu wa CWT wilaya Isdori Ndarabe amemshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa kusimamia kuziondoa changamoto za elimu. 

“Sisi hatuna ugomvi na serikali ila tunawakumbusha tu kauli yetu ya CWT kuwa haki inaenda na wajibu,hivyo tutaendelea kuwakumbusha walimu kuwa na nidhamu na watimize wajibu wao huku serikali ikiwatekelezea haki zao na kuongeza morali ya kazi,”alisema katibu huyo.

Mwenyekiti wa CWT wilaya Ladislaus Nkuu ameipongeza serikali chini ya mheshimiwa Rais Magufuli kwa moyo wake wa kizalendo na utayari wa kuwalipa madeni yao walimu kwa kuwa inawaongezea nguvu zaidi ya kutimiza majukumu yao.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania