CURRENT NEWS

Monday, February 5, 2018

HUBERT KAIRUKI KUJENGA KITUO KUSAIDIA WENYE MATATIZO YA UJAUZITO


Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Professa Charles Mgone akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano iliohusu maadhimisho ya Kumbukizi ya muasisi na Mmiliki wa Shirika la Elimu Kairuki (KHEN), Chuo Kikuu cha Kumbukumbuku ya Hubert Kairuki (HKMU), Hospitali ya Kairuki (KH) na Shule ya Uuguzi Kairuki (KSN). Mkutano huo umefanyika Dar es Salaam leo Februari 4, 2018. Kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo HKMU (Taaluma), Prof. Ntabaye Moshi na Mkurugenzi wa Hospitali ya Hubert Kairuki, Dkt. Assey Mchomvu.
Na Cathbert Kajuna- Kajunason/MMG.
Katika kuadhimisha miaka 19 ya kumbukizi ya Marehemu Profesa Hubert Kairuki, Shirika la afya na elimu la Kairuki limejipanga kujenga kituo cha kusaidia watu wenye matatizo ya kupata ujauzito kwa njia ya kawaida.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Professa Charles Mgone amesema kuwa maadhimisho hayo yaliyoanza tokea Februari 1-6, 2018 jambo kubwa wamejipanga kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kusaidia watu wenye matatizo ya kupata ujauzito kwa njia ya kawaida huko Bunju jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Ali Hapi.
"Kumekuwa na matatizo hasa ya ukosefu wa vituo vya kuwasaidia watu wenye matatizo ya uzazi jambo linalotupa msukumo wa kuanza ujenzi huu, kwa sasa tupo katika hatua za mwisho tupate kibali tuanza ujenzi maana sisi tumeshajipanga na tumeshazalisha wataalamu wa kutosha," alisema Prof. Mgone.
Professa Mgone amesema kukamilika kwa kituo hicho kitakuwa msaada mkubwa maana mpaka sasa hospitali ya Hubert Kairuki imekuwa chachu katika utoaji wa huduma ya afya ambapo kwa siku wanapokea zaidi ya wagonjwa 700.
Aliongeza kuwa mbali na ujenzi wa kituo hicho wanatarajia kuanzisha kliniki ya mama, baba na mtoto huko Bunju ili kuendeleza kuokoa vifo vya akinamama na watoto hasa waliombali na huduma.
Jambo lingine ambalo wanalifanya katika maadhimisho hayo ni kutoa huduma za afya bure kwa kipindi cha kuanzia Februari 1-6, 2018  kwenye Hospitali ya Kairuki, pia wanajitolea damu kwa hiari ili kuokoa vifo vitokanavyo na ukosefu wa damu.
Vile vile wanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu cha Hubert Kairuki watashiriki katika shindano la kujipima ujuzi juu ya mambo mbalimbali katika taaluma ya afya, maswali ya ufahamu kuhusu Tanzania, maisha ya mhasisi Marehemu Prof. Kairuki, Jiografia na jamii kiujumla.
Mwisho wa kilele cha maadhimisho hayo kutafanyika mhadhara wa kitaaluma utakaoendeshwa na Professa Malise Kaisi juu ya mada 'Maono ya Prof. Hubert Kairuki yanayodumu': Umuhimu wake katika utoaji wa huduma za afya barani Afrika.
Shirika la Afya na Elimu la Kairuki (KHEN) limasimamia Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Hospitali ya Kairuki (KH) na Shule ya Uuguzi Kairuki (KSN) ambapo muasisi wake ni marehemu Hubert Clement Mwombeki Kairuki aliyezaliwa Juni 24, 1940 Bukoba mkoani Kagera.
Mnamo Machi 17, 1987 muasisi huyo alianzisha hospitali ya TAG Mikocheni na mwaka 1992 aliibadilisha jina na kuitwa Mission Mikocheni hospitali ambayo kwa sasa inaitwa Kairuki Hospitali.
Mwaka 1997, Prof. Kairuki alianzisha Mikocheni International University na baadae miaka 2 kupita alifariki dunia Februari 6, 1999 na chuo kikabadilishwa kuwa Hubert Kairuki Memorial Univesity.
Wakati hospitali inaanzishwa ilikuwa walikuwa na uwezo wa kupokea wagonjwa wa nje 200 na wagonjwa wa ndani 30 kwa siku na kwasasa hospitali inauwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje 700 kwa siku na wagonjwa 150 wa ndani ambapo wakati muasisi anafariki chuo kilikuwa na wanafunzi 30 katika fani ya udaktari na uuguzi kwasasa chuo kinatakribani wanafunzi 1509.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania