CURRENT NEWS

Tuesday, February 6, 2018

JAFO AAGIZA UJENZI WA MADARASA SHULE YA MSINGI MWANDEGE

  
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule ya msingi Mwandege.

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule ya msingi Mwandege.

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akitoa maagizo kwa viongozi wa wilaya ya Mkuranga juu ya ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Mwandege.

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akikagua matofali yaliyoandaliwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa shule mpya ya Kipara Mpakani.

Wanafunzi wa shule ya msingi Mwandege wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo alipo watembelea shuleni hapo.
  ....................................................................


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhe.Selemani Jafo amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Mkuranga na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuanza ujenzi wa madarasa haraka iwezekanavyo katika shule ya msingi Mwandege ili kuondoa msongamano wa wanafunzi madarasani.

Agizo hilo amelitoa leo baada ya kutembelea katika Shule hiyo yenye zaidi ya wanafunzi 3700 ambapo kati yao wanafunzi zaidi ya 560 ni darasa la kwanza pekee. 

Amesema kutokana na hamasa kubwa ya jamii kuwapeleka watoto kujiunga na elimu ya msingi kwa kutumia fursa ya elimu ya msingi bila malipo kumesababisha msongamano wa wanafunzi shuleni hapo.


Aidha Waziri Jafo amewaangiza viongozi hao wa wilaya kuweka mikakati ya haraka ili kuondoa kero ya vyumba vya madarasa na madawati shuleni hapo.

Kadhalika, Jafo ameagiza ujenzi wa shule mpya katika eneo la Kipara Mpaka ambalo lipo jirani na  shule ya mwandege sambamba na kukamilisha shule mpya ya Chatembo ili kupunguza idadi kubwa ya wanafunzi waliopo kwenye shule hiyo.

Amesema baada ya shule hizo kujengwa wanafunzi hao watatawanywa katika maeneo hayo mapya.

Katika kupunguza kero hiyo ya upungufu wa nyumba vya madarasa,  Waziri Jafo amewapa hamasa walimu kwamba serikali itapeleka fedha ndani ya wiki hii ili ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa uanze haraka iwezekanavyo. 

“Ifikapo Machi 6, mwaka huu vyumba vya madarasa viwe vimekamilika na nawaonya Ofisi ya mkuu wa wilaya na Ofisi ya mkurugenzi kuacha malumbano yasiyo na maana ambayo yanarudisha nyumba upelekaji wa huduma za jamii kwa wananchi,”amesisitiza Jafo


Katika ziara hiyo, Jafo amewaomba viongozi na wananchi wa wilaya ya Mkuranga wamuunge mkono Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Abdallah Ulega kwani anajituma sana kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Mkuranga.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania