CURRENT NEWS

Friday, February 9, 2018

JAFO APONGEZA UJENZI WA MIUNDOMBINU, KITUO CHA AFYA MANEROMANGO..............................................................................................
Nteghenjwa Hosseah,OR-TAMISEMI.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Tawala za Mikoa
Mhe. Selemani Jafo amepongeza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Kisarawe kwa usimamizi madhubuti wa ujenzi wa miundombinu
ya Afya katika Kituo cha Afya Maneromano Wilayani Kisarawe.

Pongezi zilitolewa pia kwa Uongozi wa Mkoa wa Pwani kwa
usimamizi wake Makini, Utoaji wa Maelekezo na Ushauri kwa
Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu Mpango huu wa Ujenzi na
Ukarabati wa Vituo vya Afya Mkoani hapa.


Waziri Jafo ametoa pongezi hizo baada ya kupokea Taarifa ya
kukamilika kwa Ujenzi wa miundombinu ya Kituo hicho uliokamilika
kwa asilimia 99 toka kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Kisarawe.

“Nimeridhishwa sana na kazi inayoendelea ambayo itakamilika ndani
ya muda mfupi, hii inaonyesha umakini wa viongozi katika kusimamia
Mradi huu wa Afya nawapongeza sana. Nguvu na Umakini mliotumia
katika mradi huu mzihamishie  katika maeneo mengine ambayo
tunatekeleza miradi ya maendeleo; Tunataka kuona miradi yote ya
Kisarawe inatekelezwa kwa viwango vinavyohitajika ili tutatue
changamoto za wananchi” Alisema Mhe. Jafo.

Aliongeza kuwa Kituo hiki  kilipata Fedha  mwezi Septemba,2017 na
kuanza ujenzi OKtoba 2017 ambayo ilikuwa ni awamu ya kwanza ya
Ukarabati wa Vituo vya Afya 44 ambavyo vilitakiwa kukamilika
Januari 30,2018 na katika vituo vya mwanzo ambavyo vimefanya kazi
hii kwa wakati na kwa Ubora ni hiki cha Maneromango.

Waziri Jafo aliagiza vituo vingine Nchini vilivyovyopo kwenye Mpango
wa Ujenzi wa Miundombinu ya Afya kuja kujifunza katika kituo hiki
cha Maneromango kutokana na kazi nzuri iliyofanyika hapo. Pongezi 
zaidi alizitoa kwa wananchi wa maeneo yanayozunguka kituo cha
Maneromango sambamba na viongozi wao kwa ushiriki mzuri katika
kufanikisha ujenzi huo.

“Hakika, Wananchi wakishirikishwa vizuri na kuelewa mradi, mwitikio
wao huwa mkubwa na ushirikiano wao ni wa hali ya juu katika kuleta
mafanikio. Niwaombe wananchi wote mjitokeze kushiriki katika
ujenzi wa vituo vyetu vya afya vinavyoendelea kujengwa Mkoani
hapa,” alisisitiza Waziri Jafo.

Katika Taarifa ya Ujenzi wa kituo hicho ilisema kuwa Majengo
yaliyokamilika mpaka sasa ni Maabara, Chumba cha Upasuaji, Wodi
ya kina mama, Nyumba ya Mganga,Chumba cha kuhifadhia maiti,
mfumo wa kuvunia maji ya Mvua pamoja na eneo maalumu la
watembea kwa miguu(Walkways).

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa Ukamilishaji  wa miundombinu hiyo
umeenda sambamba  na manunuzi ya Samani katika majengo yote
mapya na ununuzi wa dawa na vifaa tiba kutoka Bohari ya Dawa
yaani MSD.

Vilevile, taarifa hiyo ilieleza kuwa kutokana na kukamilika kwa
nyumba ya Mtumishi  Daktari aliyepangiwa hapo amekwisha fika
kituoni na kuishi kwenye Nyumba mpya sambamba na kuanza kazi
rasmi ya kuwahudumia wananchi.

Ujenzi wa miundo mbinu katika kituo hiki cha Afya Maneromango
umegharimu kiasi fedha za Kitanzania Milioni 500 na Vifaa Tiba
viemgharimu Millioni 220.

Kutokana na Ujenzi wa Miundombinu ya Afya kukamilika kwa 99%

kituo cha Afya Maneromango kitafunguliwa rasmi siku chache zijazo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania