CURRENT NEWS

Friday, February 2, 2018

KOICA KUISAIDIA DODOMA MRADI WA UIMARISHAJI HUDUMA ZA AFYA ZA DHARURA KWA WAJAWAZITO NA WATOTO


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amekutana na kufanya Mazungumzo na Ujumbe wa Viongozi wa Shirika la Kimataifa la Misaada la Korea Kusini (KOICA) ulioongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika hilo hapa nchini Bi. Hyunsun Kim

Ujumbe huo ulijumuisha Maafisa watano (5) kutoka nchini Korea na Ofisi za KOICA hapa nchini na Wajumbe watatu (3) kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambapo Kiongozi wa Ujumbe huo Bi. Hyunsun Kim amemwelezea Dkt. Mahenge kuwa KOICA imedhamiria kutekeleza Mradi wa Uimarishaji wa Huduma za Afya za dharura kwa Wajawazito na Watoto unao tarajiwa kugharimu takribani Shilingi za Kitanzania Bilioni 14.

Aliongeza kuwa eneo la Afya ni eneo ambalo KOICA wana uzoefu mkubwa  na wamekuwa wakishiriki kwenye maeneo mengi. Alibainisha kuwa Ujumbe huo wa KOICA umewasili Mkoani Dodoma kwa lengo la kufanya upembuzi wa awali kwa kushirikiana na Timu ya Uendeshaji na Usimamizi wa Huduma za Afya Mkoa wa Dodoma kubaini mahitaji halisi ya huduma hiyo katika Mkoa na kuongeza kuwa KOICA wanaupa Mkoa wa Dodoma kipaumbele katika kutekeleza mradi huo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Daktari James Kiologwe alijulisha kuwa mradi huo utajumuisha uimarishaji wa kituo cha Damu Salama kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa kukiongezea uwezo wa kukusanya, kutunza Damu na kutengeneza Mazao mbalimbali ya Damu, Pia mradi utahusisha uimarishaji wa huduma za dharura kwa wakina mama wajawazito na huduma za watoto katika vituo vya Afya vya Mkonze kwenye Manispaa ya Dodoma, Chipanga kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na Mlowa Barabarani kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.

Daktari James Kiologwe alitaja vituo vingine vya Afya vitavyoimarishwa ni pamoja na Kituo cha Mrijo na Kituo cha Kwa Mtoro kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ambapo aliongeza kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa vyumba vya kisasa vya upasuaji, maabara, wodi na vifaa vya kisasa.

Aidha, alibainisha kuwa Mradi huo pia utahisisha kuwapatia mafunzo watoa huduma za Afya kwa akinamama wajawazito na Watoto kwenye Hospitali na vituo vya Afya vya Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo katika kutoa huduma.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alishukuru kwa msaada huo na kusema kuwa umekuja wakati muafaka kwa kuwa Afya ni moja ya masuala yaliyopewa vipaumbele kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na haswa wakati huu ambapo Serikali imehamia Mkoani Dodoma mahitaji ya huduma za Afya hususani za mama na mtoto yanaongezeka. Aidha, alitumia fursa hiyo pia kukaribisha wawekezaji kutoka Korea kuja kuwekeza Mkoani Dodoma kwa kuwa ujio wa Serikali umeambatana na fursa nyingi za Uwekezaji ukizingatia Dodoma ni katikati ya nchi.

Nae katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Ndugu Rehema Madenge ameahidi Serikali ya Mkoa itahakikisha mifumo yake yote hadi kwenye ngazi za Serikali za Mitaa inashirikiana na KOICA kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa mafanikio hapa Mkoani Dodoma

*Imetolewa na:*
*OFISI YA MKUU WA MKOA WA DODOMA*
*FEB 2, 2018*
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania