CURRENT NEWS

Thursday, February 8, 2018

MAGUFULI AMEWATENDEA HAKI WANARUFIJI KURIDHIA UJENZI WA STIEGLER'S GORGE RUFIJI - MCHENGERWA

Na Mwamvua Mwinyi,Rufiji
MBUNGE wa jimbo la Rufiji,mkoani Pwani,Mohammed Mchengerwa amesema Rais Dkt.John Magufuli hakukosea kuridhia kujengwa kwa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (stiegler's gorge) kwani utafungua milango ya kibiashara ,uchumi ,ajira na maendeleo wilayani humo.
Aidha ameeleza ataendelea kupigania kujengwa kwa barabara kutoka Nyamwage-Utete kwa kiwango cha lami , ili kuondokana na adha wanayoipata watumiaji wa barabara hiyo .
Akizungumzia utekelezaji na namna anavyoendelea kusimamia changamoto zinazowakabili wakazi wa Rufiji,katika mkutano wa wanaCCM Utete na mkoa,Mchengelwa alisema hatokata tamaa kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo .
Alisema nishati ya umeme haijafika kwenye baadhi ya maeneo lakini kutokana na ukubwa wa mradi wa stigglers gauge utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawatts 2,100 za umeme.
"Nampongeza Rais Dk.Magufuli kwa kuridhia na kuelekeza ujenzi huo ujengwe katika wilaya hii,itakuwa mkombozi mkubwa kwetu ,Na uhakika utafungua fursa nyingi za kimaendeleo na kiuchumi " alisema Mchengelwa.
Akizungumzia suala la miundombinu ya barabara ,alisema serikali imeridhia kuingiza barabara ya Nyamwage-Utete katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2018/2019 na ana uhakika itaanza ujenzi.
"Rais alifika Rufiji mwaka Jana,nilimuomba aiangalie kwa jicho la tatu barabara hii,ni ahadi yangu kwenu na kilio cha wana Utete, nitashukuru endapo ikipewa kipaombele" alisisitiza Mchengelwa.
Mchengelwa alisema, ujenzi wa barabara hiyo itasaidia ujenzi wa daraja la kuelekea Mkongo ,kwani tayari michoro imekamilika .
Kuhusu elimu, aliishawishi wizara ya elimu katika ukarabati wa shule ya sekondari Utete ambapo imetoa sh.mil 260 na ukarabati wa shule ya sekondari Muhoro ambayo imetolewa mil.180 na ukarabati unaendelea.
Kwa mujibu wa Mchengelwa,aliahidi kituo cha afya Ikwiriri kitoe huduma ya upasuaji na kujengwa ukuta na imejengwa ambapo wizara imetoa mil.700 kukarabati kituo hicho pamoja na zahanati ya Nyamwage.
Alielezea,yeye mwenyewe amechangia mifuko ya saruji 200 kwa ajili ya ujenzi kituo cha afya kikubwa katika kata ya Mwaseni na wizara inatoa mil.750 kwa ajili ya ujenzi huo .
Mchengelwa alisema ,wakati anaingia madarakani alipigania kushuka kodi ya kitanda na hatimae waziri alibadilisha sheria ambapo kodi ya kitanda ilishuka kutoka sh.120,000 hadi 20,000 inayotozwa sasa.
"Nimefanya mengi ndani ya miaka hii miwili ,wapo baadhi hawayaoni ,wengine wanadiriki kuanza kufanya kampeni sasa,wanafanya fitna na majungu kunichafulia kwa wananchi"
"Naombeni mniache nifanye kazi ,niligombea kuwatumikia wananchi lakini sio kujaribiwa,waache nihukumiwe 2020 ,huu sio wakati wa kukatishana tamaa,"alifafanua Mchengelwa.
Mchengelwa,alibainisha anaendelea kuvalia njuga ,changamoto za migogoro ya ardhi na wakulima na wafugaji.
Alisema atahakikisha anasimamia mikakati iliyowekwa na serikali ambayo itaweza kuwasaidia baina ya wakulima na wafugaji kwa kushirikiana na viongozi wa halmashauri.
Awali akiibua hoja ya kivuko,mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa (MNEC) kupitia Mkoa wa Pwani, Hajji Jumaa ,alisema wananchi wanalalamikia vivuko binafsi ambavyo vinatakiwa kukaa umbali wa km.2 jambo na haviruhusiwi kufanya kazi. 
Hajji aliomba waziri husika afikishiwe malalamiko hayo ili boti binafsi ziweze kuruhusiwi ,maana boti ya serikali haikidhi mahitaji.
Mbunge Mchengelwa na mbunge wa viti maalum mkoani Pwani ,Zainab Vullu ,walisema tatizo la  kivuko wanalijjua hivyo watalisimamia na kulibeba kulipeleka bungeni, kwenda kulifanyia kazi .
Kwa upande wake ,Mwenyekiti wa CCM Mkoani Pwani,Ramadhani Maneno ,alikemea tabia ya baadhi ya watu kuanza kufanya kampeni kabla ya mwaka wa uchaguzi mkuu.
Alisema ,tabia hiyo inalenga kuwakatisha tamaa wabunge waliopo madarakani jambo ambalo sio zuri .
Maneno alisema ,CCM Mkoa itawachukulia hatua kali wale wote ambao watawabaini wanapitapita kufanya kampeni kabla ya wakati.
Alieleza ,2020 wanachama na wananchi wenyewe watawapima viongozi waliowachagua 2015 ,na kuwapima kwa kutekeleza ahadi na kama wametekeleza ilani ya chama.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania