CURRENT NEWS

Friday, February 23, 2018

NAIBU WAZIRI MADINI AMALIZA MGOGORO WA MIAKA 7

 Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akiwa na wananchi katika utatuzi wa migogoro uliodumu kwa miaka 7.
 Naibu Waziri Stanslaus Nyongo akizungumza na wananchi.
Wananchi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini katika utatuzi wa mgogoro.
.............................................................................................................................
Sekta ya Madini imekuwa ikikabiliwa na migogoro Kati ya Wawekezaji na wachimbaji wadogo ambao wamekuwa wakifanya shughuli za uchimbaji katika maeneo mbalimbali ya Madini.
Hali hiyo imekuwa ikitokana na Wachimbaji wadogo  Nchini kuwa na tabia ya kuvamia maeneo ya wachimbaji wakubwa bila kufuata taratibu hali ambayo imekuwa ikisababisha migogoro.
Changamoto hii ya uvamizi wa maeneo na uchimbaji bila leseni ilikuwa ni tatizo kubwa kwa wachimbaji wadogo katika Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza katika eneo la machimbo ya Dhahabu ya Ishokeelaela ambapo kulikuwa na mgogoro kati ya mwekezaji mzawa Baraka Ezakieli wa kampuni ya Busolwa Mining Limited  ambae anafanya kazi uchimbaji katika eneo hilo.
Akiwa Katika Ziara yake ya kikazi, Naibu  Waziri wa Madini Stanslaus  Nyongo amemaliza mgogoro kati ya mwekezaji huyo na  wachimbaji wadogo ambao umedumu kwa muda wa miaka 7 .
Awali wananchi hao walitoa malalamiko yao  kwa Naibu Waziri huyo kuwa mwekezaji huyo amekuwa akiwazuia  kuchimba dhahabu katika maeneo ya mashamba  wanayomiliki ambayo yapo pembezoni mwa mgodi wa Buhunda  gold projety.
Akitoa ufafanuzi Afisa Madini wa kanda ya Mwanza, Yahaya Samamba alisema Mwekezaji huyo anafanya uchimbaji kihalali kwa kuwa anamiliki leseni ambayo alipatiwa na Wizara ya Madini, na kwamba tatizo lililopo ni wananchi hao wamekuwa wakichimba mita 200 kutoka katika machimbo hayo jambo ambalo kisheria hairuhusiwi kwa usalama wao kutokana ulipuaji wa miamba unaofanywa na mwekezaji.
Kufuatia maelezo hayo, Naibu Waziri  Nyongo alitembelea na kukagua mipaka ya mgodi ambapo mwananchi pekee alionekana shamba lake lipo ndani  mita 200 ni Mama Malosha  Lutamla  na Mwekezaji huyo hatakiwi kufanya uchimbaji katika mita hizo ambazo ndani yake kuna shamba la Mama huyo hadi amlipe fidia.
Kutokana na hali hiyo, Nyongo amemtaka mwekezaji huyo asiendeleze shughuli za uchimbaji katika mita 200 hizo ambazo zipo ndani ya shamba la mama huyo.
‘’Serikali inawapenda wachimbaji wadogo pia tunahitaji kuona watu waliopo ndani ya mita 200 wanakuwa salama pamoja na anayelalamikia eneo lake  mama huyu  afidiwe na mwekezaji alipwe ,’’ alisema
Aliwataka  wachimbaji wadogo  kujiunga katika vikundi vidogo ili  serikali iwasaidie wapatiwe leseni kwa sababu  kila moja anawajibu wa kufata sheria na kanuni za uchimbaji, sheria ya madini inamtaka mtu yoyote anayefanya shughuli za madini kuwa na leseni ili serikali iweze kupata kodi ambazo zitasaidia katika shughuli za maendeleo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania