CURRENT NEWS

Saturday, February 24, 2018

NAIBU WAZIRI WA MADINI AAGIZA KUTOLEWA MIKATABA YA WAFANYAKAZI MIGODINI


Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akikagua eneo la uchimbaji madini ya makaa ya mawe katika kijiji na Kata ya Magamba baada ya kuwasili kwa ziara ya kikazi kukagua miradi ya uchimbaji madini Mkoani Songwe.
Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akisalimiana na kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Mbozi mara baada ya kuwasili kwa ziara ya kikazi kukagua miradi ya uchimbaji madini Mkoani Songwe.
 Picha Zote Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog
Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akikagua eneo la uchimbaji madini ya makaa ya mawe katika kijiji na Kata ya Magamba baada ya kuwasili kwa ziara ya kikazi kukagua miradi ya uchimbaji madini Mkoani Songwe.

Na Mathias Canal, Songwe

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko ameagiza wamiliki wa kampuni za uchimbaji wa Madini kote nchini kuwapatia mikataba ya kazi wafanyakazi wote pasina kubagua.

Mhe Biteko ametoa agizo hilo Leo 23 Februari 2018 wakati alipotembelea eneo la uchimbaji wa makaa ya mawe katika Kijiji na Kata ya Magamba, Wilayani Mbozi linalomilikiwa na kampuni ya Magamba Coal Mine.

Alisema amejiridhisha kuwa wafanyakazi wengi katika migodi mbalimbali nchini ukiwemo wa Magamba hawana mikataba jambo ambalo linafifihisha uhakika wa ajira zao.

Aidha, Naibu Waziri huyo wa Madini ametoa siku 14 kuanzia Leo 23 Februari 2018 mpaka 9 Machi 2018 kwa kampuni ya Magamba Coal Mine kuwa wamekamilisha taarifa ya utekelezaji wa maelekekezo ya ukaguzi wa migodi yaliyotolewa kwao na Ofisi ya Madini kanda hiyo.

Alisema kuwa endapo watashindwa kufanya hivyo ni wazi kuwa watakuwa wamekiuka masharti ya leseni zao na wajibu wao kwa jamii inayowazunguka na hivyo Wizara itawachukulia hatua bila kuchelewa.

Sambamba na hayo pia kampuni hiyo imetakiwa kuboresha na kuwa na mahusiano chanya na kijiji cha Magamba na serikali kwa ujumla ikiwemo kusaidia kuboresha baadhi ya maeneo ikiwemo sekta ya afya na elimu.

Naibu Waziri wa Madini akiwa katika ziara ya kikazi katika Mkoa wa Songwe alisema kuwa serikali imekusudia kurejesha uchumi fungamanishi kwa wananchi hivyo kampuni haziwezi kuwa na uchumi imara kama zitasalia kuendesha migodi pasina utaratibu wa kisheria.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania