CURRENT NEWS

Thursday, February 22, 2018

NAIBU WAZIRI WA MADINI AKERWA NA USIRI WA MAPATO YA MUWEKEZAJI MGODI WA SUNSHINE


Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa mgodi wa uchimbaji madini ya dhahabu wa Sunshine uliopo Wilayani Chunya wakati wa ziara ya kikazi Mkoani Mbeya, Jana 21 Februari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza kwa ukali na baadhi ya viongozi wa Mgodi wa uchimbaji madini ya dhahabu wa Sunshine uliopo Wilayani Chunya wakati wa ziara ya kikazi Mkoani Mbeya, Jana 21 Februari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza kwa ukali na mmoja wa kiongozi wa Mgodi wa uchimbaji madini ya dhahabu wa Sunshine uliopo Wilayani Chunya wakati wa ziara ya kikazi Mkoani Mbeya, Jana 21 Februari 2018.

Na Mathias Canal, Mbeya

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko amekerwa na usiri wa mapato na matumizi ya muwekezaji wa mgodi wa uchimbaji madini ya dhahabu wa Sunshine uliopo Wilayani Chunya Mkoani Mbeya.

Mhe Biteko ameonyesha masikitiko makubwa wakati akizungumza na uongozi wa mgodi huo mara baada ya uongozi wa mgodi huo kushindwa kumpatia taarifa ya mapato na matumizi wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani humo kukagua shughuli za uchimbaji Madini.

Kumbukumbu hizo zimekosekana kufuatia viongozi wa ngazi ya juu ya mgodi kutokuwepo kwenye kikao hicho pamoja na kukiri kupokea taarifa ya ujio wake kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chunya.

Alisema kuwa viongozi hao kukosekana pamoja na kuwa na taarifa ya muda mrefu juu ya ziara hiyo ni utovu mkubwa na nidhamu kwa serikali ya awamu tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli.

Alisema kuwa pamoja na kutokuwepo kwao lakini taarifa zilitakiwa kuwepo ofisini kwani ni kosa kisheria kukosekana kwa taarifa za mgodi ilihali sheria ya Madini ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017 inaeleza vyema kuwa mmiliki wa leseni ya Madini anatakiwa kutunza kumbukumbu za mapato na matumizi kwa miaka mitano.

"Endapo atashindwa kufanya hivyo serikali itamchukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kifungo cha mwaka mmoja jela ama faini ya shilingi Milioni 50 mpaka milioni 150" Alisema Naibu Waziri huyo

Mhe Biteko akizungumza huku akionyesha kukerwa na baadhi ya viongozi ambao walikuwepo katika eneo la ofisi ya mgodi huo huku wakishindwa kuhudhuria katika kikao hicho cha kazi alisisitiza kuwa muwekezaji wa mgodi huo anapaswa kuzingatia na kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi.

Sambamba na hayo pia Mhe Biteko aliutaka uongozi wa mgodi huo kutoa taarifa sahihi za uwepo wa mashapu katika mgodi waliyokuwa wakichimba au kama mashapu katika mgodi huo yameisha wafuate taratibu za kisheria za ufungaji wa mgodi ikiwemo kuyarudisha mazingira katika halo take ya kawaida.

MWISHO.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania