CURRENT NEWS

Tuesday, February 6, 2018

RAIS DKT.SHEIN AMEZINDUA JENGO LA MAHAKAMA LA WILAYA YA MWANAKWEREKWE

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Mahkama ya Wilaya Mwanakwerekwe kutatoa fursa kwa Mahakimu watakaoitumia Mahkama hiyo kufanya kazi kwa bidii, weledi sambamba na kufuata maadili ya kazi zao.


Rais Dk. Shein ameyasema hayo leo mara baada ya kulizindua jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe, mjini Unguja baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa.Katika maelezo yake Dk. Shein aliwaeleza Mahakimu kuwa hivi sasa watafanya kazi zao kwa furaha kwani kila Hakimu atakuwa na ofisi yake tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma ambapo walikuwa wakikaa zaidi ya mmoja na kuwa kikwazo katika utendaji wao wa kazi.Alisema kuwa jengo hilo litatoa changamoto kwao kwani hapatarajiwi kuwa na ucheleweshaji wa mashauri ambao si utaratibu mzuri kwa mahakama.Dk. Shein alisema kuwa Mahkama ni chemchem ya kutoa haki na kila mtu anayekwenda Mahkamani anakwenda kufuata haki, hivyo ni juu ya Mahakimu kufanya haki katika kesi wanazozihukumu na wasikurupuke wala kubabaisha.Alieleza kuwa mara nyingi haki hukosekana kutokana na vitu vingi ikiwemo suala la rushwa ambalo Serikali yake inalipiga vita kwa nguvu zote sambamba na kuwepo suala la kujuana ambalo nalo husababisha mwenye haki kunyimwa haki na kupewa ndugu au rafiki.Aidha, alieleza kuwa Serikali ina wajibu wa kutayarisha sera na sheria zinazoimarisha na kukuza fursa ya kupata haki nchini sambamba na kuwa na wajibu mkubwa wa kuziimarisha na kuziwezesha Taasisi mbali mbali za Serikali zenye majukumu ya kutoa na kupanua fursa za kupata haki.Aliwasihi wananchi wote wasichelewe kufika Mahkamani kudai haki zao pale wanapohisi wamedhulumiwa haki zao na waepuke kwenda sehemu nyengine ambazo haziwezi kusaidia au kuweka pembeneni uamuzi uliotolewa na chombo hicho.Pia, aliwataka wananchi washirikiane na wahusika mbali mbali hasa wanapotakiwa kutoa ushahidi katika kesi za jinai zinazofunguliwa Mahkamani kuhusu kesi za ubakaji, udhalilishaji dawa za kulevya na nyenginezo. “ushahidi ni jambo muhimu sana unaosaidia hukumu ifanyike kwa haraka”,alisisitiza Dk. Shein.Pamoja na hayo, Dk. Shein aliiagiza Wizara ya Nchi Afisi ya Rais, Katiba, Sheria na Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha inajenga haraka jengo la Mahkama Kuu huko Tunguu ambapo mnamo mwaka 2020 yeye mwenyewe akalizindue tena si zaidi ya hapo kwani mda haupo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania