CURRENT NEWS

Friday, February 23, 2018

UWAMAMI KISARAWE WALALAMIKIA FAINI NA TOZO KANDAMIZI KATIKA BIASHARA ZAO

 Baadhi ya wafanyabiashara wa mazao ya misitu wilayani Kisarawe ,wakiwa wameambatana kumuona ofisini kwake mkurugenzi wa halmashauri ya Kisarawe ,Musa Gama kwa ajili ya kuwasaidia kutatua kero ya tozo wanazotozwa katika usafirishaji ushuru wa mazao.
 Mkurugenzi wa halmashauri ya Kisarawe, Musa Gama , akitoa ufafanuzi kuhusu malalamiko yaliyotolewa na wafanyabiashara wa mazao ya Misitu Kisarawe (UWAMAMI),;:mwenye fulana ya kijani wanaotazamana na mkurugenzi ni mwenyekiti wa UWAMAMI ,Ally Mnemvu.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Mfanyabiashara wa mazao ya misitu wilayani Kisarawe,Pwani ,Ashura Dando, akitoa malalamiko kuhusu kizuia cha Kauzeni, ambacho kinadaiwa kuwazidishia vipimo na ujazo ukilinganisha na vizuia vingine 

Na Mwamvua Mwinyi,Kisarawe
WAFANYABIASHARA wa mazao ya misitu wilayani Kisarawe mkoani Pwani ,(UWAMAMI)wamekilalamikia kizuia cha Kauzeni, ambacho kinadaiwa kuwazidishia vipimo na ujazo ukilinganisha na vizuia vingine pamoja na kuwatoza faini ya sh.200,000 hali ambayo inawaumiza kibiashara .

Aidha wamemuomba mkurugenzi wa halmashauri ya Kisarawe ,kuwasaidia kutatua kero ya tozo za ushuru wanazotozwa na idara ya fedha wakati wa kusafirisha mazao ,;tozo ambazo zinakinzana na zile za serikali kuu.

Kutokana na hali hiyo , baadhi ya wafanyabiashara hao ,walikwenda ofisini kwa mkurugenzi huyo kumueleza juu ya utata wa kuongezewa ujazo ,kuzidishiwa vipimo ,faini na tozo wanazolipishwa.

Mwenyekiti wa UWAMAMI Ally Mnemvu, alisema wao wanahudumiwa na ofisi mbili tofauti ikiwemo halmashauri na wakala wa misitu(TFS ) hivyo wanaomba ushirikiano wao kutatua matatizo hayo .

"Qubimeter inapima magogo,kuni na mbao na hamuwezi amini cubimeter ikizidi moja tunalipishwa 200,000 ,chakushangaza utapita vizuizi vyoteee Kurui na kwingine ujazo unaweza ukawa 10 lakini ukifika Kauzeni tuu lazima vipimo vizidi kisha unapigwa faini "alisema Ally.

Akizungumzia tozo za ushuru wa usafirishaji mazao alisema, kipindi cha nyuma serikali kuu ilikuwa ikiwalipisha sh.16,600 kwa ujazo wa kilo 75  na gunia huku halmashauri ikilipisha sh .1,600 .

Ally alisema baadae serikali ilibadilisha ujazo wa usafirishaji wa mkaa wa kilo 50 inatakiwa halmashauri iwatoze kwa asilimia tano lakini idara ya fedha bado inawalipisha 1,600 kwa ujazo huo.

Mwenyekiti huyo ,alisema lengo lao ni kutaka kupewa elimu ya kisheria ili kuwekana sawa katika masuala ya sheria.

Alisema wao kama wafanyabiashara wanahitaji msaada wa kujulishwa kuhusiana na tozo na faini wanazolipishwa lakini isiwe faini kandamizi.

Wafanyabiashara wa mazao hayo ,Shomvi Ally na Mohammed Muombo walisema hakuna mfanyabiashara anaenusurika faini kwenye kizuizi hicho .

"Ujazo kwingine unakuta upo sawa lakini kizuizi kinachopeleka mapato idara ya fedha halmashauri ya Kisarawe kipimo kinakuwa kikubwa ,sasa haijulikani kipimo chao ni kibovu ama ,haiwezekani ujazo au vipimo vikatofautiana " alisisitiza  Shomvi.
 "," Hatujajua sheria zao zinatofautiana wapi wakati serikali ni moja ,itakuaje halmashauri iliyo chini ya serikali iwe na sheria zake tofauti na sheria zilizowekwa na serikali ";alisema Muombo.
Ashura Dando, alielezea yeye alipofika kizuia cha Kauzeni aliombwa rushwa na akakataa kutoa ndipo alipoambiwa mzigo wake wa kuni umezidi kuni tano alipie faini 200,000 .

Alisema amelipia kibali sh.326,600 hawadaiwi , wanalipa kodi ,hivyo hawana tatizo na halmashauri ,wala hawakatai kutozwa faini ila wanaomba kizuizi cha Kauzeni kichunguzwe.
" Kuna mtoza faini pale almaarufu anaitwa Magumashi,ukifika tuu pale ni balaa anakwambia mtu huna kibali wakati unacho na anaomba rushwa ,halmashauri, isimamie hilo .ilihali wafanyabiashara tuondokane na kadhia hii."alieleza Ashura.
Nae mkurugenzi wa halmashauri ya Kisarawe, Musa Gama ,alisema kati ya malalamiko yote waliyomueleza amegundua kuna tatizo katika upimaji ,ujazo unatofautiana wakati wakisafirisha biashara zao.
Aliagiza zikakae mezani pande zote tatu , wakala wa Misitu (TFS) Kisarawe ,halmashauri na UWAMAMI ili kujua kikwazo kipo wapi na namna ya kupata ufumbuzi.

Hata hivyo ,Gama alieleza kuhusu faini zote zipo kwa mujibu wa sheria kwa yeyote atakaekiuka taratibu.

Alifafanua sheria ya fedha za serikali za mitaa ilifanyiwa marekebisho mwaka 2017 ambapo ilibadilisha viwango vya chini vya utozaji tozo za adhabu kutoka 50,000 hadi 200,000 -milioni moja jambo ambalo wafanyabiashara hao wanapaswa kulielewa.


Mkurugenzi huyo aliruhusu waandishi wa habari wakamuone mwanasheria wa halmashauri ya Kisarawe ili kupata ufafanuzi wa sheria zaidi suala ambalo mwanasheria huyo hakuonyesha ushirikiano kwani aliitwa mgambo kuwafukuza waandishi hao na kushindwa kufanikisha walichokihitaji.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania