CURRENT NEWS

Monday, February 5, 2018

VIJIJI NA VITONGOJI KIBITI NA RUFIJI VYATAKIWA KUANZISHA MADAFTARI YA TAARIFA ZA WAKAZI ILI KUBAINI WATU WASIO WEMA

Na Mwamvua Mwinyi,Kibiti

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Pwani, Ramadhani Maneno, amezitaka serikali za vijiji,vitongoji wilayani Kibiti na Rufiji, kuanzisha madaftari ya taarifa za wakazi ambayo yatasaidia kuwatambua wageni ili kukabiliana na hali ya ulinzi na usalama kwenye maeneo hayo .

Aidha amewahimiza wananchi katika wilaya hizo ,kuendelea kulinda amani na utulivu, ili hali kuinua maendeleo ambayo yalididimia katika kipindi cha mpito cha matukio mbalimbali ya kiuhalifu na mauaji.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 41 ya CCM yaliyofanyika kimkoa ,Wilayani Kibiti,Maneno alisema matukio hayo, yalisababisha wanachama kupunguza imani na chama chao kwa kujenga hofu na mashaka.

Alieleza madaftari ya wakazi yatawezesha kujua wakazi wapya,wageni na kuwafuatilia ambao wanatiliwa shaka kuwa si watu wema katika eneo husika.

Maneno alisema yapo madhara ya kukaribisha wageni ambao hawafuatiliwi ujio wao wala taarifa zao kujua walipotokea.

"Atakaetaka kuwa rafiki na watu wa aina hiyo asije kutulaumu,vyombo vyetu vinafanyakazi usiku na mchana" alifafanua Maneno.

Hata hivyo alivipongeza vyombo na vikosi vya ulinzi na usalama ambavyo bado vipo imara na anashukuru hali kwa sasa ipo shwari.

"Nachukua nafasi hii kuwapa pole ,wale wote ,mlioguswa na tatizo hilo kwa namna moja ama nyingine,wengine walikimbia makazi yao,na wengine kuacha ofisi zao ,

" Baadhi ya wanachama waliogopa hata kuvaa sare za chama ,na kusita kujitanua kujivunia kwa mazuri yanayotekelezwa nchini kupitia utekelezaji wa ilani ya CCM ,:;Kwasasa fanyekazi zetu za kujiinua kiuchumi na kimaendeleo ,na sisi CCM Mkoa tupo nyuma yenu"alisema Maneno.

Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Pwani,alitoa rai kwa CCM ngazi zote za chini kuhakikisha wanaanzisha miradi mbalimbali ili kuondokana na tabia ya kuwa ombaomba na utegemezi .

Nae mkuu wa wilaya ya Kibiti ,HusseinGulam Kifu alisema, serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama inaendelea kudhibiti hali ya amani na utulivu wilayani hapo .

Aliwaomba wananchi kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake na kufichua wale ambao wanawadhania sio watu wema.

Kifu alisema, vyombo vya ulinzi na usalama vinatekeleza wajibu wake na jamii inapaswa kushirikiana navyo kwa kutoa taarifa za wahalifu katika maeneo yao ili wachukuliwe hatua zinazostahili .

Kwa upande wake ,mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa kupitia mkoa wa Pwani (MNEC) Hajji Jumaa, aliiasa jamii kumuunga mkono mwenyekiti wa CCM Taifa ,na Rais Dk.John Magufuli na kupambana na umasikini kwa kufanya kazi.

Alisema,viongozi wa chama wabadilike waache tabia ya kukaa maofisi bali waende kusikiliza kero za wananchi na kuwaeleza yale yanayotekelezwa na serikali .

Hajji ,alielezea huu ni wakati wa mabadiliko ya kimaendeleo,ni lazima kila kiongozi akimbizane na kasi ya Dk.JPM.

Awali, katibu wa CCM wilaya ya Kibiti Zena Mgaya,aliishukuru CCM mkoa kuhitimisha kilele cha maadhimisho ya miaka 41 ya chama hicho wilayani humo.

Alisema, wapo kwenye ujenzi wa ofisi ya chama wilaya hivyo wanawaomba wadau kuendelea kuchangia ili kukamilisha ujenzi huo haraka.

Katika madhimisho hayo ,mbunge wa jimbo la Kibiti Ally Ungando alishachangia ujenzi huo kwa gharama ya sh.Mil.5.2 na aliahidi kuweka madirisha ya vioo ,kamati ya siasa ya CCM mkoa ilichangia sh.500,000 na mbunge viti maalumu mkoa wa Pwani, Zainabu Vullu alichangia malumalu (vigae).

Wengine ni chama cha ushirika cha korosho Mkoani Pwani- CORECU -kimeahidi kutoa sh.300,000 na kampuni ya utafiti ya madini ya kinywe (URANEX )iliyopo Lindi ambayo ilitoa mifuko ya saruji 100 .
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania