CURRENT NEWS

Monday, March 12, 2018

ALEX MSAMA: TUKUTANE CCM KIRUMBA TAMASHA LA PASAKA APRILI MOJA
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion Bw. Alex Msama akizungumzia maandalizi ya Tamasha la Pasaka litakalofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba Aprili 1 Jijini Mwanza na Aprili 2 Uwanja wa Halmashauri mjini Bariadi mkoani Simiyu huku akiwatangaza baadhi ya waimbaji katika tamasha hilo kushoto ni mwimbaji Beatrice Mwaipaja na kulia ni Mwimbaji Paul Clement.
Beatrice Mwaipaja kushoto na Mwimbaji Paul Clement. wakizungumza na waandishiwa habari kuhusu maandalizia ya Tamasha la Pasaka.
................................................................................. 
Na Said Mwishehe, Globu ya Jamii

APRILI Moja katika Uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza,macho na masikio ya Watanzania yataelekezwa uwanjani hapo.Kwanini jibu ni moja tu kutakuwa na Tamasha la Pasaka.

Tamasha la Pasaka ambalo limekuwa likiandaliwa na Msama Promotion kila mwaka na kufanyika siku ya Sikuu ya Pasaka.Ni tamasha ambalo limekuwa likiwaweka Watanzania pamoja.

Ni tamasha ambalo msingi wake mkubwa ni kudumisha upendo na mshikamano kwa Watanzania na kila mwaka kumekuwa na kauli mbiu kuhusu tamasha hilo.

Kwa kukumbusha tu kauli mbiu kwenye tamasha la Pasaka kwa mwaka jana ilikuwa inasema hivi "Umoja na upendo kudumisha amani ndani ya nchi yetu" ...na lilifanyika jijini Dar es Salaam, Mwanza na mikoa mingine kwa siku tofauti .

Tamasha la Pasaka la mwaka huu ambalo sasa linafanyika Mwanza kwa mara ya kwanza kauli mbiu yake inasema “UMOJA NA UPENDO HUDUMISHA AMANI KATIKA NCHI YETU” na sababu kubwa ni kwamba Msama Promotion inataka kuwahubiria injili ya Amani na Upendo wakazi wa Kanda ya Ziwana na Vitongoji vyake.

Ukweli ni kwamba msingi mkuu wa Tamasha la Pasaka ni kutumia tamasha hilo kwa ajili ya kuabudu na kumtukuza Mungu.Hivyo ni tamasha ambalo linahusisha zaidi waimbaji wa nyimbo za Injili huku waalikwa mbalimbali wakiwemo viongozi Maaskofu na wachungaji wakitoa jumbe nyingi za kuhumiza Upendo, Amani na Utulivu kwa watanzania.

Kampuni ya Msama Promotioni kupitia Mkurugenzi wake Alex Msama imekuwa ikifanya jitihada za kuhakikisha wanaohudhuria tamasha hilo wanaburudika  kutokana na aina ya waimbaji ambao hupata nafasi ya kutumbuiza kwa kuimba nyimbo za Injili katika tamasha hilo.

Waimbaji wengi maarufu wa muziki huo kutoka ndani na nje ya Tanzania wamekuwa wakishiriki kila mwaka kwenye Tamasha la Pasaka.Tamasha ambalo mwaka huu ni la 18 tangu kuanzishwa kwake

Kadri miaka inavyosonga mbele ndivyo ambavyo umaarufu wake unazidi kuongezeka.Kwanini? Jibu ni kwamba Watanzania wamekuwa wakisubiria kwa hamu tamasha hilo kila mwaka na limekuwa ni Baraka tosha kwa maisha yao na familia zao mbele ya Mungu.

Msama na Kampuni yake imefungua milango sahihi ya Watanzania kupata sehemu ya kwenda siku ya Pasaka na si kwingine bali ni kwenye tamasha la Pasaka.Hivyo jamii ya Watanzania na hasa yenye hofu ya Mungu imekuwa ikitamani kuona siku ya Tamasha la Pasaka inafika ili kujumuika na wenzao wengine kushuhudia uponyaji wa mungu kutoka kwa waimbaji wa nyimbo za Injili.

Hongera Msama kwasababu umetambua katika maisha ya binadamu kuna njia nyingi za kumfanya kuwa karibu na Mungu wake hasa kwenye sikukuu ambazo kimsingi zinatokana na imani za dini.Sikukuu ya Pasaka huadhimishwa kila mwaka baada ya Wakristo duniani kote kumaliza Kwaresma kwa siku 40 ambayo huhitimishwa kwa sikukuu ya Pasaka.

Ukweli ni kwamba Tamasha la Pasaka limekuwa na historia ya aina yake nchini kwetu.Wakati linaanza lilionekana kama tamasha la kawaida lakini kama ambavyo nimeeleza hapo juu sasa kila mmoja wetu analichukulia kwa uzito wa aina yake.

Zipo sababu nyingi lakini kubwa zaidi ni tamasha ambalo pamoja na kwamba limekuwa likitumika sehemu ya kutumbuiza wananchi wanaofika kwenye tamasha hilo kwa kupata nafasi ya kushuhudia waimbaji wa nyimbo za Injili.

Akizungumzia tamasha la Pasaka kwa mwaka huu Mkurugenzi wa Msama Promotion Alex Msama anasema ni la kipekee sana kwasababu ni kwa mara ya kwanza linafanyika Kanda ya Ziwa tangu kuanzishwa kwake miaka kadhaa iliyopita.

"Hii ni fursa pekee kwa watu wa Kanda ya Ziwa na vitongoji vyake katika burudani , kupata baraka za Mungu lakini kuwaunganisha Watanzania pamoja.

"Kwa kutumia tamasha la Pasaka mbali ya kutoa burudani inayoambana na ujumbe wenye kumpendeza Mungu, pia hutoa nafasi ya Watanzania kumkaribia Mungu zaidi na kubwa zaidi kufurahia sikukuu ya Pasaka tukiwa wamoja,"anasema Msama.

Msama anasema kila baada ya kumalizika kwa mTamasha la Pasaka kiasi cha fedha zinazopatikana zimekuwa zikitumika katika kulipia karo za baadhi ya watoto yatima katika vituo vya kulelea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu lakini pia zimekuwa zikisaidia kutoa misaada ya mahitaji maalum ikiwemo chakula katika vituo hivyo ili nao wajisikie ni miongoni mwa watu wanaoshiriki kikamilifu katika msima wa Tamasha la Pasaka

Anafafanua kuwa Aprili 1 mwaka huu Tamasha la Pasaka litafanyika Uwanja wa CCM Kirumba likitumbizwa na waimbaji mbalimbali wa muziki wa Injili kutoka mataifa mbalimbali.

"Aprili 2 mwaka huu tamasha hilo lifanyika Bariadi mkoani Simiyu kwenye Uwanjwa wa Halmashauri.Hivyo kwa mwaka huu tamasha hilo litafanyika huko Kanda ya Ziwa tofauti na miaka yote ambapo limekuwa likianzia katika Jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine ikiwamo ya Mbeya, Iringa na Morogoro,"anasema Msama.

Kwa kuwakumbusha tu Watanzania kwa mwaka huu baadhi ya waimbaji wa muziki wa Injili watakaotumbuiza siku ya tamasha hilo ni Rose Mhando ambaye pia atatumia tamasha hilo kuzindua albamu yake.

Pia watakuwepo Upendo Nkone , Christopher Mwahangira, Beatrice Baraka, Matha Mwaipaja, Ephraim Sekereti kutoka nchini Zambia, Solomon Mkukubwa kutoka Kenya, Faraja Ntaboba kutoka DR Congo , Paul Crement, Jesca Honore, Angel Bernard, wengine wengi.

Kwa mazingira ya aina hiyo , hakuna sababu ya mkazi wa Kanda ya Ziwa kuanza kutafakari na kuumiza kichwa wapi pakwenda.Huna sababu kwani tayari Msama Promotion tayari amekurahisishia.

Msama bado anasisitiza kuwa wakazi wa Mwanza na Simiyu kujiandaa kwa ajili ya kuhudhuria tamasha hilo kwa mwaka huu wa 2018.

"Njooni kwenye tamasha la Pasaka mwaka , mje mpokee baraka.Tupo kwa ajili ya kuhakikisha Watanzania wanapata burudani ya muziki wa Injili na kila mwaka limekuwa na mvuto wa aina yeke.Karibuni nyote kwani ni tamasha ambalo hufanyika mara moja kila mwaka na sasa ni zamu ya Kanda ya Ziwa,"amesema Msama.

Binafsi naungana na Msama.Naomba niwe balozi wake wa kuzungumzia tamasha la Pasaka kwa kuwaomba wakazi wa Kanda ya Ziwa kuwa uwepo wapo wao siku hiyo ni muhimu kama ambavyo Msama ameona umuhimu wa kulipeleka tamasha hilo huko.Najua mikoa mingine nako wanalisubiri na kwa kuwa limekuwa likifanyika kila mwaka huenda mwakani litakuwa mkoani kwako.

Nihitimishe kwa kusisitiza kuwa Aprili Moja mwaka huu wakazi wa Kanda ya Ziwa na hasa mikoa ya Mwanza na Simiyu tukutane CCM Kirumba na Uwanja wa Halmashauri Bariadi kwa ajili ya  Tamasha la Pasaka
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania