CURRENT NEWS

Wednesday, March 7, 2018

ALIYEKUWA DIWANI WA KATA YA GIHANDU,WILAYANI HANANG AJIUZULU NA KUJIUNGA NA CCM

Na Jumbe Ismailly -HANANG . 


ALIYEKUWA diwani wa kata ya Gihandu,wilayani Hanang,Mkoani Manyara kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo,Mathayo Samuhenda amejiuzulu udiwani wa kata hiyo na kujiunga na Chama Chama Mapinduzi (CCM)

Akitangaza azma yake hiyo ya kujiuzulu katika nafasi yake ya udiwani wa kata hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Gihandu,Samuhenda alisisitiza kwamba aliamua kujiuzulu na kuwaacha wapiga kura wake siyo kwa njia ya ukatili bali alifikia maamuzi hayo kwa lengo la kuwaunganisha wananchi wote wa kata hiyo.  

Aidha alifafanua kwamba katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili sasa wananchi wa kata hiyo wana matatizo ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kutokana na wanasiasa kutumia mtaji huo kuomba kura.
“Inatosha wanasiasa sisi tutumie shida ya maji ili tuoate kura tuondoke,inatosha..na watu wa Gihandu nawaomba sana hiyo ikiletwa kama sehemu ya mnada mzuri tu wa mtu kujinadi mkataeni inatosha tumeumia vya kutosha.”alisisitiza Samuhenda. 

Hata hivyo diwani huyo aliyejiuzulu aliweka bayana kwamba umefika wakati sasa kwa wanasiasa kubadili ajenda za kupatia kura za Gihandu na isiwe upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwani hiyo sasa imekuwa ni kejeli

Akimpokea diwani huyo,Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara,Simon Lulu alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaoendeleza makundi licha ya kuwa hivi sasa siyo wakati wa kumpeni na badala yake aliwataka kuvunja makundi hayo na kusisitiza juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo alisisitiza pia kwamba suala la kuvunja makundi siyo la hiyari bali ni la lazima kutokana na makundi hayo baadhi ya wanachama mchana wanakuwa CCM huku usiku wanatumikia Vyama vya upinzani.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Hanang,Methew Darema alimpongeza diwani huyo kwa kitendo chake cha ujasiri cha kujiuzulu nafasi aliyokuwa nayo pamoja na kwamba ni hivi karibuni alitembelewa na kiongozi wake wa kitaifa kwa lengo la kuhamasisha watu kujiunga na chama hicho.

Kwa upande wake baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Gihandu,Stephano Ngudu alisema mwaka 2008 kila mwananchi alichangia shilingi 86,500/= kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari na Hosteli mbili,lakini mpaka leo hakuna ujenzi wowote wa majengo hayo uliokamilika na fedha walizochanga hawajarudishiwa.
 Ni Mbunge wa Jimbo la Hanang,Mkoani Manyara,DK.Mary Nagu (wa kwanza kutoka kushoto) akimpongeza aliyekuwa diwani wa Kata ya Gihandu,Mathayo Semuhenda mara baada ya kutangaza azma yake ya kujiunga na CCM.
 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara,Simon Lulu akipokea kadi ya Chama Cha ACT Wazalebdo kutoka kwa aliyekuwa diwani wa kata ya Gihandu,Mathayo Semuhenda.
 Aliyekuwa diwani wa kata ya Gihandu kwa tiketi ya ACT Wazalendo,MATHAYO SEMUHENDA akipokea kadi ya CCM baada ya kutangaza azma yake ya kujiunga na CCM.
 baadhi ya viongozi wa chama cha mapinduzi (CCM) wa wilaya na Mkoa wa Manyara wakishiriki kikamilifu pamoja na wanachama wapya kula kiapo cha uadilifu baada ya kuwakabidhi kadi za chama wanachama wapya wa chama hicho.
Aliyekuwa diwani wa kata ya Gihandu,Mathayo Semuhenda akila kiapo cha uadilifu mara baada ya kukabidhiwa kadi ya chama cha mapinduzi(ccm)

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania