CURRENT NEWS

Saturday, March 17, 2018

JAFO AWAAGIZA WAKUU WA MIKOA KUBUNI MIKAKATI YA KUONDOA TATIZO LA OMBAOMBA MIJINI.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda katika uzinduzi wa Utalii wa jiji la Dar es salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo akizungumza na wananchi katika Uzinduzi wa Mpango wa Utalii wa Jiji la Dar es salaam.


Kikundi cha sanaa kikitumbuiza kwa wananchi walioshiriki uzinduzi wa Mpango wa Utalii wa Jiji la Dar es salaam.

Baadhi ya wananchi walioshiriki uzinduzi wa Mpango wa Utalii katika jiji la Dar es salaam.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda pamoja na viongozi mbalimbali na wasanii katika uzinduzi wa Utalii wa jiji la Dar es salaam.
 ....................................................................................................


Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo amewataka wakuu wa mikoa kubuni mikakati ya kuondoa tatizo la ombaomba mijini.

Waziri Jafo aliyasema hayo alipokuwa akizindua Mpango wa Utalii wa Jiji la Dar es salaam ambao umelenga kuvutia watalii mbalimbali kwa kutumia fursa zilizopo ndani ya jiji hilo.

Katika uzinduzi huo, Jafo amesema ombaomba hao wamekuwa wakikaa barabarani hali ambayo haileti sura nzuri kwa nchi na kwa wageni mbalimbali wanaokuja kutalii nchini.

Waziri Jafo amesema changamoto ya watoto wa mitaani na tatizo kubwa la ombaomba ni vyema wakuu hao wakabuni mbinu mbalimbali zikiwemo za kuwawekea maeneo maalum ya kujihusisha na shughuli za ufugaji na kilimo cha bustani ili kuwaondoa mitaani.

“Tukifanya hivi tutakuwa tumefanikiwa kuondokana na kitendo cha wao kukaa barabarani kwa kuwa hakileti sura nzuri kwa nchi yetu kwa wageni mbalimbali wanaokuja kutalii hapa nchini,”amesema Jafo.
 
Awali akimkaribisha Waziri Jafo, Makonda amezitaka Manispaa za Mkoa huo kuimarisha usafi kwa kuwa suala la utalii lazima liendane na mazingira nadhifu ya jiji la Dar es salaam.

Kadhalika, Makonda amepiga marufuku tabia ya kukamatwa kwa wasanii wanaorekodi video za nyimbo au movie kwenye maeneo ya jiji la Dar es salaam kwa kuwa linarudisha nyuma utalii na kwamba wasanii hao wamekuwa wakisaidia kutangaza jiji hilo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania