CURRENT NEWS

Thursday, March 1, 2018

OR-TAMISEMI YAENDA SAMBAMBA NA TAFITI ZA NBS


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akifungua kikao cha Uwasilishaji wa Takwimu za Utoaji wa huduma za Afya ya Msingi kwa mama na mtoto zilizowasilishwa na Ofisi ya Taifa ya  Takwimu kupitia Jukwaa la kukusanya na kuchambua Takwimu za Afya na Lishe “NEP”.

 Kaimu Meneja wa Takwimu za Mazingira kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi.Ruth Minja(Katikati) akiwasilisha Salamu za Taasisi hiyo kabla ya kuwasilisha Takwimu za Utoaji wa huduma za Afya ya Msingi.
  Baadhi ya Wakurugenzi wa OR-TAMISEMI wakifuatilia uwasilishaji wa Takwimu za Utoaji wa huduma za Afya ya Msingi kwa Mama na Mtoto.
 Mtafiti Mkuu wa Sayansi kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia Dr.Khadija Malima akiwasilisha mada kuhusu huduma za Kliniki kwa wajawazito katika kikao cha kuwasilisha Takwimu za Utoaji wa huduma za Afya ya Msingi.
 Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Ndg.Mrisho Mrisho akichangia hoja wakati wa Kikao cha Uwasilishaji wa Takwimu za Utoaji wa huduma za Afya ya Msingi.
Katika Picha ya pamoja ni Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe.Selemani Jafo(mbele Katikati), Naibu katibu Mkuu Elimu Tixon Nzunda(mbele kushoto), Kaimu Meneja wa Takwimu za Mazingira,NBS Bi.Ruth Minja pamoja na wadau kutoka NEP.
.......................................................
Angela Msimbira, OR-TAMISEMI.

Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na  Serikali za Mitaa kuanzia mwaka 2015-2018 imetekeleza kwa kiasi kikubwa matokeo ya tafiti iliyofanywa na  Ofisi ya Taifa ya Takwimu “NBS” kupitia Jukwaa la kukusanya na kuchambua Takwimu za Afya na Lishe “NEP” iliyofanyika Mwaka 2005-2015.

Akizungumza katika ufunguzi wa Kikao cha kuwasilisha taarifa hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali  za Mitaa Mhe.Selemani Jafo amesema matokeo hayo yamejikita katika Mpango kazi wa Wizara hii tangu Serikali ya Awamu ya tano ilivyoingia madarakani.

Aliendelea kusema katika eneo la Miundimbinu ya Afya ambayo imeonekana katika Tafiti kuwa haikithi mahitaji ya wananchi kwa kutokuwa na huduma muhimu kama vile kuwa na Wodi za Mama na Mtoto, huduma za upasuaji na sambamba na uhaba wa wataalamu wa Afya ambapo kwa sasa Wizara inaendelea na maboresho makubwa katika Sekta ya Afya kwa ujumla wake.

“ Hapo awali tulikuwa na Vituo vya Afya 586 ambavyo  vilivyokuwa vinaweza kutoa huduma za Upasuaji ni 120 tu lakini  hivi sasa tumeweza kukarabati vituo 205 ambavyo vyote vitatoa huduma ya upasuaji, vitakuwa na wodi ya mama na mtoto, vichomea taka, chumba cha kuhiadhia maiti, maabara pamoja na Wataalamu wa Afya” Alisema Jafo.

Hivyo kwa kiasi kikubwa tumetembea kwenye matokeo ya Tafiti hii inayowasilishwa leo na tuna uhakika kwenye Tafiti ijayo matokeo yatakuwa tofauti na yalivyo sasa tunajivunia jitihada hizi na tunawapongeza Ofisi ya  Taifa ya  Takwimu kwa matokeo haya.

Wakati huo huo Mhe. Seleman Jafo amewaagiza Watafiti nchini kuwa waadilifu katika kutafuta na kutoa Takwimu sahihi ili Serakali iweze kujitathmini na kuweka mikakati katika utoaji wa huduma katika jamii na kuleta maendeleo.

Amesema kuwa Takwimu zikiwa sahihi na kuandikwa kwa weledi husaidia katika kuleta maendeleo kwa jamii kwa kupanga bajeti zenye uhalisia kulingana na takwimu zilizotolewa ambazo zinaonyesha mapungufu yaliyopo na jinsi ya kutatua mapungufu hayo.

“Takwimu husaidia kupanga mikakati mbalimbali  ya kuleta maendeleo katika Taifa hivyo ni vyema zikawa sahihi na zinazolinda maslahi mapana ya taifa kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.” Amesema Jafo


 Halkadhalika Mhe. Jafo amesemaTakwimu hii imeipa Wizara mwelekeo ya kujipima kulingana na kazi mbalimbali za Afya zinazoendelea kufanyika katika maeneo yote Nchini.

Wakati huohuo Bi. Ruth Minja Kaimu Meneja wa Takwimu za Mazingira kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) amesema   National Evaluation Platform (NEP) ni  Jukwaa ambalo linakusanya na kuchambua takwimu za afya na Lishe kutoka vyanzo mbalimbali ili kuwezesha Serikali kupata majibu ya kimkakati  ya ushahidi ya kitakwimukatika utekelezaji wa Sera na Programu zote zinazohusu afya ya lishe  ya Mama Mjamzito na Mtoto.

Amesema NEP linajumuisha mkusanyiko wa mbinu mbalimbali za kitakwimu ambazo zinawasaidia wafanya maamuzi kuainisha maswali ya kipaombele na kuyafanyia tathmini.

Aidha amebainisha kuwa Uchambuzi umekusanya taarifa muhimu  ambazo zinasaidia kutambua kuwa ni afua zipi za afya  zinafanya vizuri na kubainisha mapungufu  katika utendaji ili kuweka mbinu  na kubuni njia ya kuboresha huduma ya mama na motto katika Lishe.

Kikao  cha kupokea  matokeo ya utafiti wa huduma za afya Nchini iliyowasilishwa na  Jukwaa la kukusanya na kuchambua takwimu za afya na Lishe ( National Evaluation Platform-NEP)  na kusimamiawa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa NBS kimefanyika leo  katika ukumbi wa TAMISEMI mjini Dodoma.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania