CURRENT NEWS

Thursday, March 22, 2018

UHAMISHO WA WALIMU SEKONDARI KWENDA SHULE ZA MSINGI SIO ADHABU


   Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI (kushoto) akiongozwa Mwenyekiti wa Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya anayestaafu Bibi Mayasa Hashimu (Kulia) kuingia kwenye ukumbi wa Chuo cha Mipango kwa ajili ya kufunga mkutano wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya.
 Afisa Elimu wa mkoa wa Pwani bwana Abdul Maulid (kulia) aliyekaa mstari wa mbele akiwa pamoja na Maafisa wenzake wa Elimu wa Mikoa na Wilaya wakimsikiliza mgeni rasmi Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe.Joseph Kakunda (hayupo) pichani wakati wa ufungaji wa Mkutano wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya.

 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bibi Paulina Nkwama akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI kufunga Mkutano wa Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya.
    Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe Joseph Kakunda akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya nchini.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe Joseph Kakunda akimpongeza Bibi Dyness mosha ambaye ni mmoja wa Maafisa Elimu wanaostaafu mwaka huu.

...............................................................
Na Mathew Kwembe, TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amesema uamuzi wa Serikali kuwahamisha baadhi ya Walimu wa shule za Sekondari wanaofundisha masomo ya sanaa kwenda kufundisha shule za Msingi ulilenga kukabiliana na upungufu mkubwa wa walimu uliopo katika shule za Msingi nchini na kamwe siyo adhabu.
Katika hotuba yake Waziri Jafo iliyosomwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Joseph Kakunda katika mkutano mkuu wa tano wa mwaka wa Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya Tanzania Bara jana mjini Dodoma,ametaka maafisa elimu hao kuwapanga walimu kwa vigezo vilivyoweka na serikali na sio kama adhabu.
Amema kamwe maafisa elimu wasiwapangie walimu hao wa sekondari kwenda shule ya msingi kwa kigezo cha kutoa adhabu kwa walimu bali wazingatie vigezo hivyo.
Waziri huyo amesema ameshaagiza kuwa kigezo cha mikondo ndio kiwe kigezo sahihi cha kupanga walimu.
“Nitalisimamia kwa karibu sana suala hili, pia kigezo cha kupanga walimu shule za msingi kwa kutumia idadi ya wanafunzi kinazinyima shule zenye wanafunzi wachache kuwa na walimu wa kuweza kufundisha darasa la Awali hadi darasa la saba kwa ufanisi.

“Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe.Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua kuwa upo upungufu wa walimu kwa shule za msingi na walimu wa sayansi kwa shule za sekondari,” amesema.

Kwa mujibu wa Waziri Jafo, amesema  kuna upungufu wa walimu wa shule za msingi 85,000 nchini wakati ziada ya walimu wa masomo ya sanaa katika shule za sekondari ni 21,000.
Waziri Jafo amesema kulingana na takwimu hizo serikali imeona ni vema walimu hawa wa masomo ya sanaa wapelekwe kufundisha shule za msingi kwani uamuzi huo wa serikali umezingatia suala la matumizi mazuri ya rasilimali watu.
Amesema kutokana na wingi wa walimu wa sanaa katika shule za sekondari mwalimu mmoja wa sanaa alikuwa akifundisha chini ya vipindi 10 kulinganisha na mwalimu wa sekondari ambaye alikuwa akifundisha vipindi 20.

Aidha Waziri Jafo pamoja na kutambua kuwepo kwa upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo kwa upande wa msingi na sekondari, ameziagiza halmashauri zote 185 kuweka nguvu katika kukamilisha miundombinu ya shule za Msingi na Sekondari pamoja na maabara.

Pia Waziri Jafo amewaagiza Makatibu Tawala  wa Mikoa pamoja na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza agizo la kununua magari na kutenga fedha za ununuzi wa magari kupitia bajeti za Mikoa na Halmashauri.

Kuhusu wahitimu wa Darasa la saba wa mwaka 2018 kupata vyeti vyao, Waziri Jafo amesema kuwa serikali imelichukua ombi hilo kwa uzito unaostahili.

Katika risala yake, Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya Bibi Mayasa Hashimu ameiomba serikali iwasisitize wakurugenzi wa halmashauri kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari kwa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya.


Pia ameiomba serikali kuweka msisitizo wa pamoja katika usimamizi wa ujenzi na ukarabati wa Matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa, maabara na hosteli shuleni.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania