CURRENT NEWS

Wednesday, April 4, 2018

WANANCHI WA CHEMBA WATAKIWA KUJUA HAKI ZAO ZA MSINGI ZA KISHERIA

Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Ndg.Jofrey Pima

................................................................................................
Na Shani Amanzi,

Wananchi wa Wilaya ya Chemba washauriwa kuhakikisha wanafahamu haki zao za kisheria ,pale wanapoona zimekiukwa na mtu binafsi,Serikali au Shirika lisilo la Kiserikali na kutambua kuwa hiyo haki inaweza patikana sehemu gani.

Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Ndg.Jofrey Pima aliyazungumza hayo alipokuwa ofisini kwake tarehe 03/4/2018 na kutaja baadhi ya migogoro ya ardhi iliyopo katika Halmashauri kuwa imegawanyika katika makundi matatu na kuelezea njia zipi zinatumika katika kutatua migogoro.

Ndg.Pima amesema migogoro ya Mipaka kati ya Wilaya ya Chemba na Wilaya jirani kama vile mgogoro wa mpaka uliowahi kutokea Wilaya ya Kiteto, Chemba na Bahi,Chemba na Singida mfano hai ni mgogoro wa Mpaka unaolalamikiwa na Wananchi wa Kijiji cha Handa Wilaya ya Singida kuwa Wanachi wa Handa wamevamia hifadhi ya Msitu wa Migori.

“Kwa hiyo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Chemba na ya Wilaya ya Singida walishakutana na kutatua huo mgogoro, changamoto nyingine inayosababisha migogoro ya mipaka, ni maboya (becons) kutoonekani kwa sababu baadhi ya wananchi wanang’oa maboya hayo na baadhi ya
maboya kuwa mbalimbali changamoto ambayo inatakiwa kutatuliwa kwa kupunguza umbali kati ya boya moja na nyingine zinazoonekana kiurahisi ”alisisitiza Ndg.Pima.

Aidha Ndg.Pima amesema migogoro mengine ni mgogoro ya mipaka baina ya vijiji na vijiji katika wilaya tofauti mfano ni kijiji cha Kidoka na kijiji cha Muungano kata ya Kidoka katika Wilaya ya Chemba wanalalamikia baadhi ya Wanachi wa Viijiji vya Haneti na Kwahenu Wilaya za Chamwino kuingia kwenye maeneo ya Vijiji hivyo vya Chemba. 

Mgogoro huu ulishaanza kushughulikiwa na Wataalam kwa kubaini mipaka na Tamko la mipaka itatolewa na Wakuu wa Wilaya za Chemba na
Chamwino muda si mrefu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Dkt.Semistatus Mashimba aliongeza kwa kusema kuna migogoro ya umiliki wa Ardhi ambayo hutatuliwa na Wataalam wa Halmashauri na mengine inapelekwa kwenye vyombo vya kisheria ambavyo vimepewa mamlaka ya kushughulikia migogoro ya Ardhi ,Mabaraza ya Kata na Baraza la Ardhi la Wilaya ya Kondoa kutegemea thamani ya ardhi yenye mgogoro.

“Migogoro inayoletwa moja kwa moja Ofisini kwangu au kwa Mkuu wa Wilaya hushughulikiwa kwa kushirikisha Mwanasheria wa Halmashauri na Wataalam wa Ardhi, na endapo itaonekana mgogoro
huo unatakiwa kuamriwa na Mahakama wahusika huelekezwa kupeleka mgogoro huo kwenye Mahakama yenye Mamlaka ya kusikiliza mgogoro husika.”alisisitiza Dkt.Mashimba.

Hata hivyo Malengo ya Halmashauri ni kutatua migogoro yote ya Wananchi waliyonayo katika Sekta ya Ardhi na Sekta Nyingine kama vile Kilimo na Mifugo, Mirathi na Ndoa.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania