CURRENT NEWS

Saturday, May 12, 2018

KASI YA MKANDARASI ANAYEJENGA BARABARA ZA MJI WA GEITA YAMKERA JAFO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo akisomewa taarifa ya ujenzi wa barabara za mji wa Geita.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo akikagua barabara zilizojengwa katika mji wa Geita.

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo akikagua soko la kisasa lililojengwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri ya mji Geita.

Eneo la soko la kisasa katika mji wa Geita.

Ujenzi wa jengo la Halmashauri wa mji wa Geita linalojengwa
............................................................
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo amekerwa na kasi isiyo ridhisha ya mkandarasi anayejenga barabara za mji wa Geita na kumuagiza ifikapo julai 15 mwaka huu ahakikishe amekamilisha barabara, mifereji pamoja na taa za barabarani.


Jafo ametoa agizo hilo leo katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo kwenye mkoa wa Geita ambapo amesema serikali haiwezi kuvumilia uzembe wa aina yeyote utakaojitokeza kwenye ujenzi huo.


"Nitakapokuja tena nikute barabara zote ziwe zimekamilika pamoja na mifereji yote na taa zote za barabarani kwani serikali haiwezi kuvumilia uzembe wowote utakaojitokeza,"amesisitiza.


Aidha, katika ziara hiyo Waziri Jafo amefanikiwa kutembelea pia mradi wa soko la kisasa linalojengwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri ya wilaya ya Geita pamoja na kutembelea ujenzi wa Ofisi mpya ya Halmashauri ya mji huo.  


Katika ukaguzi huo,Waziri Jafo amefurahishwa na ujenzi wa soko zuri la kisasa na maendeleo mazuri ya ujenzi wa Ofisi mpya ya Halmashauri. 


 Hata hivyo Jafo ameagiza Halmashauri kuhakikisha wafanyabiashara wote waliokuwa wakiuza bidhaa hapo awali wawe watu wa kwanza kupewa vibanda vya kufanyia biashara zao kabla ya watu wengine wapya.


 Pia Jafo ameonya tabia ya watendaji wasio waaminifu kuzuia vibanda kwa lengo la kuvikodisha kwa bei kubwa kwa wafanyabiashara. 


Pamoja na hayo Waziri Jafo amempongeza Mkuu wa mkoa wa Geita Robert Gabriel pamoja na Mbunge wa Jimbo la Geita Constantine Kanyasu kwa jitihada zao za kusukuma maendeleo ya Halmashauri kwa kasi.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania