CURRENT NEWS

Saturday, May 19, 2018

MTATURU AKABIDHI KADI ZA MATIBABU KWA WAZEE 2500

 Mmoja wa wazee akipokea kadi ya matibabu kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu.
 Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akipita wodini kuwafariji wagonjwa waliolazwa katika kituo cha afya cha Ihanja kama sehemu ya maadhimisho hayo.
 Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akimkabidhi dokta Mapunda fedha taslimu kiasi cha shilingi 100,000 kwa ajili ya kumsaidia mgonjwa aliyelazwa hospitali ya Malkia wa Ulimwengu Puma ambaye ameshindwa kulipia gharama za matibabu.
 Baadhi ya Wajumbe wa bodi ya afya na wageni waalikwa wakimsikiliza mgeni ramsi mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu wakati akitoa hotuba kwenye maadhimisho hayo.
 Mkuu wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu akizungumza katika sherehe ya siku wauguzi duniani ambayo kiwilaya imefanyika katika kituo cha afya cha Ihanja.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akikabidhi kadi ya matibabu kwa mmoja wa wazee.
Baadhi ya wauguzi wakimsikiliza mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu katika maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani ambayo kiwilaya yalifanyika katika kituo cha afya cha Ihanja.

........................................................

KATIKA kusherehekea siku ya wauguzi duniani mkuu wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu amewakabidhi wazee wapatao 2,500 kadi za matibabu bure huku akiagiza ndani ya mwezi mmoja vituo vyote vya afya wilayani humo visivyo na dirisha maalum la kuhudumia wazee wawe wamefungua dirisha hilo.

Agizo hilo linaendana na Sera ya Afya iliyopo inayohimiza kuwa na dirisha maalum la matibabu kwa ajili ya wazee.

Akizungumza katika sherehe hizo ambazo kiwilaya zimefanyika katika kituo cha afya cha Ihanja  Mtaturu amesema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) inahimiza pia  kuwajali na kuwahudumia wazee.

"Nawapongeza wauguzi kwa kazi nzuri na ngumu mnayoifanya ya kuwahudumia wagonjwa, siku hii mkiwa mnamkumbuka mwanzilishi wenu Florence Nightingale mnapaswa kuendelea kuwahudumia wagonjwa wakiwemo wazee wetu kwa upendo na uadilifu mkubwa,"alisema mkuu huyo.

Mbali na kutoa kadi kwa wazee mkuu huyo wa wilaya amezindua rasmi bodi ya afya ya wilaya na kuwataka wajumbe wa bodi hiyo kuwa waadilifu na wabunifu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora wakati wote.

"Bodi hii ni chombo muhimu sana na kipo kisheria na nyinyi ndio waratibu na wasimamizi wa masuala yote ya utoaji afya nawaomba mkawe waadilifu na wabunifu, msiwe watu wa vikao tu piteni muone huduma zinazotolewa kwenye vituo vyetu kama ni za kuridhisha,"alisisitiza Mtaturu.

Aidha ameielekeza bodi hiyo kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii(CHF) iliyoboreshwa ambayo itaongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba na uhakika wa matibabu wakati wote ambapo
gharama yake ni sh 30,000 kwa kaya ikiwa na  wategemezi 6.

Amesisitiza pia kuhusu chanjo mbalimbali zinazotolewa na kuwaomba wananchi kuhakikisha wanapata chanjo hizo kwa kuwa zikitolewa vizuri zitasaidia kupunguza mzigo wa gharama za dawa.

"Serikali ya awamu ya tano chini Rais Dokta John Pombe Magufuli imedhamiria kuendelea kuongeza bajeti ya afya ili kuwafanya wananchi wawe wenye afya njema hivyo kuwawezesha mzalishe mali na uchumi wa Taifa ukue, hivyo ni wajibu wetu wananchi kuunga mkono jitihada hizi,"alisisitiza mkuu huyo.

Akisoma risala katibu wa Chama Cha Wauguzi Tanzania (TANA)wilayani humo Oliver Njoka ameeleza changamoto walizonazo ikiwemo uchache wa wauguzi unaofanya mzigo wa kazi kuwa mkubwa na kutopandishwa madaraja.

Akijibu changamoto hiyo Mtaturu amewapa moyo kwa kuwaomba wawe wavumilivu kwa kuwa hivi karibuni serikali imetangaza nafasi za ajira elfu 6,180 hivyo ni imani yake kuwa katika ajira hizo na wao watapata mgao ili kupunguza upungufu uliopo.

Awali akimkaribisha mgeni ramsi mwenyekiti wa halmashauri Ally Mwanga amemshukuru mkuu huyo kwa  kukubali kuwa mgeni rasmi na kwa kuisaidia halmashauri kwa mambo mbalimbali katika kutatua changamoto zinazoikabili halmashauri.

Utoaji huo wa kadi za matibabu kwa wazee hao umefanyika baada ya halmashauri  kufanya sensa wilaya nzima ili kujua idadi ya wazee waliopo huku dhamira ikiwa ni kutoa kadi kwa wazee wote waliopo katika wilaya hiyo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania