CURRENT NEWS

Saturday, May 5, 2018

NZUNDA AAGIZA HOJA ZA UKAGUZI MWISHO 30, JUNI 2018.


 Naibu Katibu Mkuu OR TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Tixon Nzunda, akifungua kikao cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Seksheni za Serikali za Mitaa sambamba na Mipango na Uratibu jijini Dodoma, kulia ni John Cheyo, Mkurugenzi wa Sera na Mipango OR TAMISEMI na kushoto ni Betrice Kimoleta Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa OR TAMISEMI. Kikao kikiwa kinafunguliwa huku wajumbe wakiwa makini kusikiliza na kunukuu maelekezo muhimu.


Kamishna wa Bajeti Dkt. Charles Mwamaja kutoka Wizara ya Fedha na Mipango akiwasilisha mada katika kikao cha makatibu Tawala wasaidizi juu ya Muongozo wa kuandika Miradi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
   ........................................................
Na, Atley Kuni, OR TAMISEMI

Serikali imezitaka Sekretarieti za Mikoa kuzisimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa kukamilisha Majibu ya Hoja zote za ukaguzi za mwaka wa fedha 2015/2016 na 2016/2017 na kuwasilisha majibu hayo kwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ajili ya uhakiki kabla ya tarehe 30 Juni, 2018.

Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Ndugu Tixon Nzunda wakati akifungua Kikao Kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi kutoka Seksheni za Mipango na Uratibu pamoja na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Seksheni za Usimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Sekretarieti za Mikoa kilichofanyika Mei 4, 2018 katika Ukumbi wa Video Conference, OR-TAMISEMI.

Nzunda ameyasisitiza hayo kufuatia agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kuwa Mikoa yote ni lazima sasa ijipange kuhakikisha inasimamia ipasavyo kazi ya kujibu hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili ifikapo muda uliotolewa na serikali hoja zote za ukaguzi ziwe zimejibiwa ipasavyo na kuwasilishwa katika mamlaka husika.

Mbali na kuwataka kusimamia ipasavyo suala la kujibu hoja, Naibu katibu Mkuu aliwaambia Makatibu Tawala hao juu ya mwenendo wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/19 ambapo alisema kuwa Bajeti katika Mamlaka za Serikali za Mitaa iliandaliwa kupitia mfumo wa PlanRep iliyoboreshwa (PlanRep Web Based), ambao umewezesha Halmashauri zote 185 kuwa na Mipango iliyoboreshwa.

Nzunda amewataka Watendaji pia kusimamia kazi za mamlaka za Serikali za
Mitaa kwa kufuata Sheria, Taratibu na Miongozo iliyopo bila ya kuwaonea haya
Wakurugenzi wa Halmashauri.

“Mkurugenzi kwa mujibu wa utendaji anawajibika kwa RAS, na wewe unapotekeleza majukumu yako unakuwa umevaa kofia ya RAS, hivyo sitegemei Katibu Tawala Msaidizi katika ngazi ya Mkoa atoe visingizio kuna Mkurugenzi anamkwamisha katika kutekeleza wajibu wake” alisema Ndugu Nzunda na kuongeza kuwa katika awamu ya sasa hakuna wakuachwa kwa kushindwa kutimiza wajibu wako.

Naibu Katibu Mkuu amefafanua kuwa katika kikao hicho watajadili kwa kina vipaumbele vya bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 ambavyo ni pamoja na Kuboresha Miundombinu ya kutolea huduma za Afya, Elimu na Maji, Kuongeza Mapato ya ndani ya Halmashauri, kuanzishwa kwa fursa za miradi ya kimkakati, Maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,  Majengo ya utawala kwa Halmashauri mpya sambamba na ununuzi wa Magari ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya.

Maeneo mengine ya Bajeti ni Ununuzi wa Boti za kutolea huduma kwenye maeneo yenye changamoto za usafiri wa majini, kutenga maeneo ya uwekezaji hususan viwanda vidogo, vya kati na vikubwa sambamba na kutenga fedha kwa ajili ya Vijana na akina Mama na watu wenye ulemavu huku nguvu kubwa ikiwekwa katika sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani ya Halmashauri.

Akitoa maelezo ya awali, Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa OR TAMISEMI, Bibi Beatrice Kimoleta alisema kuwa Seksheni ya Mipango na Uratibu pamoja na
Seksheni  inayosimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa ni kiungo muhimu katika suala zima la Masuala ya Mipango na Bajeti.

“Lazima mtambue kwamba hizi Idara mbili ninyi ndio injini ya Katibu Tawala Mkoa katika kumshauri juu ya masuala mazima ya Mipango na Bajeti. Kamwe huwezi kuzitenganisha Idara hizi halafu ukafanikiwa hivyo shabaha ya kuwaleta pamoja katika kikao hiki ni kutaka muwe na uelewa wa pamoja ili mtakapotoka hapa mkalete matokeo chanya kwenye Mikoa na Halmshauri zenu” amesema Kimoleta.

“Katika mwaka wa fedha 2018/19 Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zimepanga kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi 6,186,418,709,500 kati ya fedha hizo, shilingi 298,346,001,000 ni kwa ajili ya Sekretarieti za Mikoa sawa na asilimia 5% na Mamlaka za serikali za Mitaa ni shilingi 5,888,072,708,500 sawa na asilimia 95%” alisema

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania