CURRENT NEWS

Thursday, May 3, 2018

SERIKALI YAAHIDI KUIKARABATI SHULE YA SEKONDARI YA WASICHANA IRINGA


 Mabweni ya wanafunzi katika shule ya sekondari ya wasichana Iringa
 Wanafunzi wa shule ya wasichana Iringa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)Selemani Jafo.
 Wanafunzi wa shule ya wasichana Iringa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)Selemani Jafo.
  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)Selemani Jafo akikagua miundombinu ya shule ya sekondari ya wasichana Iringa.

Jiko la shule ya sekondari ya wasichana Iringa
.............................................................................................
Na Atley Kuni OR TAMISEMI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)Mhe. Selemani Jafo ameahidi kuwa shule ya sekondari ya Wasichana Iringa iliyopo mkoani Iringa itafanyiwa
ukarabati ikiwa ni muendelezo wa serikali wa kuzikarabati shule zake kongwe
hapa nchini.

Waziri Jafo alitoa kauli hiyo jana wakati akiwa njiani kurudi Dodoma akitokea
mkoani Iringa ambako alihudhuria sherehe za Mei Mosi na ufunguzi wa hospitali ya Wilaya ya Kilolo.

Akiwa njiani, Waziri Jafo alilazimika kufanya ziara ya kushtukiza shuleni hapo, ili aweze
kujionea hali ya miundombinu mbalimbali katika shule hiyo iliyoanzishwa tangu mwaka
1967.

Katika ziara hiyo, Jafo alikagua Mabweni, Vyoo, Bwalo la Chakula, Jiko na Ofisi za Walimu na kisha kufanya mazungumzo na walimu, watumishi wasio walimu wanafunzi sambamba na

wananchi wanaozunguka eneo la shule hiyo.


Akizungumza na walimu, watumishi wasio walimu pamoja na wanafunzi wa shule
hiyo mara baada ya kujionea hali ya miundombinu ya shule hiyo, Jafo
alieleza kuwa shule hiyo ni miongoni mwa shule kongwe zilizo kwenye mpango
wa ukarabati mkubwa ili kuwa na mazingira bora ya kusoma na kujifunzia.

“Katika mwaka wa fedha wa 2017/18 tulikarabati shule kongwe 43 na
katika mwaka huu wa 2018/19, shule hii pamoja na zingine kongwe 45
hapa nchini zitakuwa katika mpango kamambe wa kukarabatiwa kama
tulivyokwisha fanya kwenye shule kama 43 za awali ambapo shule 89 zote
kongwe tuwe tumezimaliza” alisema Waziri Jafo.

Aliongeza kuwa shule ya Wasichana Iringa imekuwa ni moja ya shule bora na
hivyo kufanya wanafunzi wengi kupenda kuhamia kwenye shule hiyo.

Sambamba na ukarabati huo Mhe. Jafo ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zote
ambazo ziliainishwa mbele yake ikiwepo upungufu wa walimu wa Fizikia na
Hisabati pamoja na stahiki za walimu.

“Mama yetu Nkondola amewasilisha changamoto za walimu wa Hesabu na Fizikia
lakini pia maslahi ya walimu, naomba nieleze kuwa suala hilo nimelichukua lakini
niwaahidi kutuma wataalam kutoka kwenye wizara yangu pamoja na wizara
nyingine za kisekta kuja kufanya tathmini ya kina juu ya haya mliyoniambia,”
alisema waziri Jafo.

Aliwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii huku akitoa ahadi  kwa jumuiya hiyo
kuwa endapo katika mitihani yao ya mwisho ya kidato cha sita watapata daraja la
kwanza (DV.1) zaidi wanafunzi ya 30 atawandalia sherehe ndogo ya kujipongeza na wale watakaopata daraja la kwanza kati ya pointi 3-5 wataalikwa bungeni kwa
gharama zake yeye.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania