CURRENT NEWS

Monday, June 11, 2018

HALMASHAURI ZAAGIZWA KUITUMIA VIZURI MIFUMO YA KIELEKTRONIKI


 Baadhi ya Waweka hazina, Wahasibu na Maafisa Wasimamizi wa Fedha kutoka Mikoa ya Mara na Kigoma wakimsikiliza Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Kamishna wa Polisi Diwani Athuman wakati akifungua mafunzo ya siku nne ya Mfumo wa Epicor toleo la 10.2
 Baadhi ya Waweka hazina, Wahasibu na Maafisa Wasimamizi wa Fedha kutoka Mikoa ya Mara na Kigoma wakimsikiliza Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Kamishna wa Polisi Diwani Athuman wakati akifungua mafunzo ya siku nne ya Mfumo wa Epicor toleo la 10.2
 Baadhi ya wawezesha kutoka Mradi wa PS3 wakifuatilia ufunguzi wa mafunzo ya siku nne ya Mfumo wa Epicor toleo la 10.2 kwa Waweka hazina, Wahasibu na Maafisa Wasimamizi wa Fedha kutoka Mikoa ya Mara na Kigoma yaliyofanyika mjini Bukoba.
  Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Kamishna wa Polisi Diwani Athuman akifungua mafunzo ya siku nne ya Mfumo wa Epicor toleo la 10.2 kwa Waweka hazina, Wahasibu na Maafisa Wasimamizi wa Fedha kutoka Mikoa ya Mara na Kigoma yaliyofanyika mjini Bukoba.
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Kamishna wa Polisi Diwani Athuman akifungua mafunzo ya siku nne ya Mfumo wa Epicor toleo la 10.2 kwa Waweka hazina, Wahasibu na Maafisa Wasimamizi wa Fedha kutoka Mikoa ya Mara na Kigoma yaliyofanyika mjini Bukoba.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Kamishna wa Polisi Diwani Athuman (aliyeketi wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Waweka hazina, Wahasibu na Maafisa Wasimamizi wa Fedha kutoka Mkoa wa Kigoma
...........................................................................................
Na Mathew Kwembe, Kagera

Watendaji wa Halmashauri nchini wameagizwa kuitumia vizuri mifumo mbalimbali ya kielektroniki iliyowekwa na Serikali kwa kushirikiana na Mradi wa PS3 katika halmashauri zote 185 nchini ili mifumo hiyo iweze kufanya kazi yake kwa malengo yaliyokusudiwa.

Agizo hilo limetolewa leo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Kamishna wa Polisi Diwani Athuman wakati akifungua mafunzo ya siku nne ya Mfumo wa Epicor toleo la 10.2 kwa Waweka hazina, Wahasibu na Maafisa Wasimamizi wa Fedha kutoka Mikoa ya Mara na Kigoma yaliyofanyika mjini Bukoba.

Alisema kuwa mifumo hii imetumia fedha nyingi kuisimika na hivyo watendaji wa halmashauri hawana budi kulijua hilo na kuhakikisha kuwa wanaitumia katika kuboresha utendaji wao wa kazi na pia kuiwezesha serikali kutekeleza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi.

Katibu Tawala huyo alisema kuwa ipo mifano kwa baadhi ya halmashauri katika mkoa wake ambazo watendaji wake wamekuwa wakishindwa kutekeleza majukumu yao vizuri.

Alisema kuwa halmashauri nyingi nchini zimewekewa mfumo wa ukusanyaji mapato lakini mifumo hii haitumiki kwa kiwango kilichokusudiwa.

Alisema halmashauri zimenunua vifaa vya kukusanyia mapato (POS) kwa ajili ya kuboresha ukusanyaji na kudhibiti udanganyifu na hila wakati ukusanyaji mapato lakini baadhi ya halmashauri zimeweka vifaa hivyo stoo.

Pia alisema kuwa uchunguzi walioufanya katika baadhi ya halmashauri za mkoa wake wamebaini kuwa baadhi ya watendaji wa halmashauri wasio waaminifu wamekuwa wakikusanya mapato kwa kutumia vifaa hivyo vya kielektroniki lakini fedha zinaishia mifukoni kwa watendaji hao.

“Mfano hapa Kagera tuna halmashauri ambazo pamoja na kuwekewa mifumo hii ya ukusanyaji mapato zimeshindwa kuitumia mifumo hiyo kukusanya mapato vizuri,” alieleza.

Akitolea mfano wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe, Kamishna Athumani alisema kuwa uongozi wa mkoa wa Kagera umelazimika kutuma wataalamu kutoka taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa kwenda katika halmashauri hiyo ili kufanya uchunguzi wa uhakiki wa mifumo yao ya ukusanyaji mapato.

Hivyo Katibu Tawala huyo aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kutoka Mara na Kigoma kuhakikisha kuwa wanayatumia vizuri mafunzo hayo kwenda kuboresha utendaji wao wa kazi.

Aidha Kamishna Diwani aliwataka Wakurugenzi wa halmashauri nchini kuhakikisha kuwa wanatekeleza wajibu wao vizuri.

Alisema kuwa watendaji wa halmashauri hawana budi kujitafakari kama wanazitendea haki taaluma zao pale wanapotekeza majukumu yao kwani ni wajibu wao kuhakikisha kuwa wanatenda haki kwa umma kwa kutekeleza vizuri majukumu waliyopewa.

Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa PS3 mkoa wa Kigoma Bwana Simon Mabagala alieleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watendaji hao kutambua maboresho yaliyofanywa na serikali ya kuwa na mfumo mmoja wa usimamizi wa fedha za umma.

Mwakilishi wa washiriki wa mafunzo Bibi Mercy Swai ambaye ni Mwekahazina wa halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kutoka mkoani Kigoma alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwao kwani yatawawezesha kumudu kuutumia mfumo wa Epicor ulioboreshwa.

Aliongeza kuwa matoleo yaliyopita yalikuwa na changamoto mbalimbali lakini mfumo wa Epicor toleo la 10.2 utawawezesha kuondokana na changamoto zilikuwepo katika mifumo iliyopita ya Epicor.


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania