CURRENT NEWS

Sunday, June 10, 2018

JAFO AMUAGIZA MKANDARASI KUBOMOA SAKAFU ILIYOJENGWA CHINI YA KIWANGO


 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) Selemani Jafo  akifanya ukaguzi wa vyumba vya madarasa katika sekondari kongwe ya Malangali ambapo ameagiza sakafu kufumuliwa kutokana na kutokuwa na ubora.
 Viongozi wakifanya Ukaguzi wa miundombinu inayojengwa katika kituo cha afya  Malangali
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) Selemani Jafo  na Mbunge wa Viti Maalum Ritta kabati walipo watembelea akina mama waliojifungua katika hospitali ya Frelimo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) Selemani Jafo  akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza,  Mbunge Ritta Kabati pamoja na wafanyakazi wa hospitali ya Frelimo.
..................................................................................................
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) Selemani Jafo amemuagiza mkandarasi anayekarabati shule kongwe ya sekondari ya Malangali iliyopo wilayani Mufindi mkoani Iringa kubomoa Sakafu iliyowekwa kwenye madarasani kutokana na kuwa chini ya kiwango.

Hali hiyo imetokea leo wakati Waziri Jafo alipokuwa mkoani Iringa katika ukaguzi wa miradi ya maendeleo.

Akiwa katika ziara hiyo, Waziri Jafo amefika katika shule hiyo na kukagua moja ya darasa ambalo tayari lilikuwa limekamilika na kubaini kuwa sakafu yake imewekwa chini ya kiwango baada ya kugonga gonga kwa viatu na kutokea nyufa.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Jafo amemuagiza Mkandarasi huyo kubomoa sakafu hiyo na kuanza kazi upya.

Jafo ameoneshwa kukerwa na hali hiyo na kuagiza msimamizi wa kazi hiyo ambaye ni Wakala wa Majengo nchini(TBA) kuhakikisha sakafu hiyo inavunjwa na kujengwa upya katika ubora unaotakiwa.

Shule ya Malangali ni miongoni mwa shule kongwe 89 ambazo serikali imeamua kuzikarabati upya ili zirudi katika ubora wake.

Katika hatua nyingine, Waziri Jafo ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi kwa usimamizi mzuri wa ukarabati kituo cha afya Malangali ambapo majengo yake yamejengwa kwa ubora wa hali ya juu.

Aidha, Jafo ameitembelea hospitali ya Frelimo iliyopo Manispaa ya Iringa na kujionea changamoto zinazoikabili hospitali hiyo ambazo zimekuwa zikiwasilishwa mara kwa mara bungeni na Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Ritta Kabati.

 Kutokana na changamoto hizo, Jafo amesema hospitali hiyo inapaswa kupewa kipaumbele kwa upande wa majengo ya Wodi pamoja na jengo la uchunguzi ili iweze kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania