CURRENT NEWS

Saturday, June 9, 2018

'LPO' ZA MAKARATASI KUTOTUMIKA KUANZIA JULAI MOSI

 Ng'wananyamate Mgengeli  Mtaalam Mshauri  kutoka mradi wa PS3, akichangia mada wakati wa mafunzo ya maofisa Manunuzi kuhusu mfumo wa Epicor 10.2 yaliyofanyika katika ukumbi wa Victoria Palace jijini Mwanza (Picha na Atley Kuni- OR TAMISEMI)
 Baadhi ya Maafisa Manunuzi wakimsikiliza kwa makini, mwezeshaji Stanslaus Msenga hayupo pichani wakati wa mafunzo jijini Mwanza (Picha na Atley Kuni OR TAMISEMI)
Stanslaus Msenga, Mhasibu Mwezeshaji akitoa somo kwa Maafisa Ugavi wa Halmashauri za Mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Geita, Tabora na Simiyu wakati wa Semina ya mfumo wa Epicor 10.2 jijini Mwanza (Picha na Atley Kuni- OR TAMISEMI) 

...........................................................................
Na. Atley Kuni- OR TAMISEMI

Wataalam wakufunzi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa wamesema
mikataba ya manunuzi (Local Purchasing Order LPO), itafikia ukomo mara baada ya kuanza
kutumika kwa mfumo wa uhasibu na uaandaji hesabu za serikali (Epicor 10.2) ifikapo 01 Julai,
2018.

Akizungumza wakati wa mahojiano maalum Mhasibu mwezeshaji Melkizedeck Kimaro kutoka
Ofisi ya Rais TAMISEMI, wakati wa mafunzo ya maOfisa manunuzi yanayowashirikisha
maOfisa kutoka Halmashauri za mikoa ya Mwanza, Simiyu, Tabora, Mara, Geita na Kagera
alisema serikali katika kurahisisha utendaji kazi na kuondokana na matumizi ya karatasi kuanzia
Mwezi Julai, 2018 taratibu zote za manunuzi zitakuwa zikifanyika kwa kutumia mfumo.

“Lengo la Serikali ni kuondokana na LPO za Makaratasi ndio maana unaona hivi sasa maOfisa
manunuzi wanapatiwa mafunzo, kabla ya hapa mpango wa manunuzi ulitumia karatasi nyingi
ambazo kwa kiasi fulani zilikuwa hazina umadhubuti katika uhifadhi wake lakini pia kukosewa
kosewa kwa makaratasi na kuwafanya kutumia makaratasi mengi” anasema Kimaro.

Kimaro amesema kuwa katika mfumo wa Epicor 10.2 itasaidia pia suala la udhibiti wa vifungu,
ambapo kila kifungu kilicho bajetiwa kwa mwaka husika ndicho kitakacho kutumika kufanya
manunuzi kwa njia ya kieletroniki na kwamba itamlazimu Ofisa manunuzi kujiridhisha juu ya
uwepo wa fedha katika fungu husika kabla yakuanza kwa mchakato wa manunuzi.

“Katika utaratibu wa sasa Ofisa Manunuzi anaweza kufanya mchakato wa manunuzi bila hata
kuangalia kama kwenye kifungu husika kinafedha na anapofikia mwisho anapotaka kufanya
malipo anajikuta hana fedha katika kifungu, lakini tutakapo anza kutumia Epicor 10.2 suala hilo
linakwenda kuondoshwa” alisisitiza Kimaro

Wataalam hao wanasema katika utaratibu wa sasa, kutamwezesha Ofisa manunuzi, mbali ya
kufanya manunuzi vilevile itamwezesha kuupokea mzigo (Receipt entry) aliouagiza kupitia
mfumo huo ambao umebuniwa na kusanifiwa na wataalam wa ndani.

Naye Emelda Malima Mkufunzi Mwezeshaji kutoka OR TAMISEMI, yeye anasema kwamba
kupitia mfumo wa Epicor 10.2 utawezesha upatikanaji wa taarifa za robo mwaka, nusu mwaka
na hata mwaka mzima kwa urahisi na wepesi.

“Kupitia mfumo huu kila jambo linalofanyika, litakuwa linanakiliwa katika mfumo na pindi Ofisa
manunuzi anapohitaji taarifa sio lazima kuanza kukusanya makaratasi na kuanza
kuyaunganisha ili apate taarifa badala yake kupitia mfumo ataweza kupakua taarifa husika
kulingana na mahitaji yake” alifafanua Emelda.

Mfumo huo pia unaelezwa kuwa ni ‘Web Base system’ inayotoa fursa kwa wataalam watumiaji
kuweza kufanya kazi zao mahali popote pale walipo tofauti na sasa ambapo katika Epicor 9.5
na zingine zilizotangulia hazikuwa na uwezo huo.

Akizungumzia mafunzo hayo yanayo endelea jijini mwanza, Meneja mradi katika mradi wa PS3
mkoani humo Bw. Pelestian Masai, alisema matokeo ya maboresho ya mfumo yalitokana na
mahitaji ya watumiaji kupitia changamoto zilizo kuwepo hapo awali.

“Maboresho ya mifumo ni suala endelevu, kikubwa hapa ni suala la mahitaji (requirements)
kutoka kwa watumiaji, walicho kifanya wasanifu mfumo (Programmers) ni kuangalia

changamoto za kimfumo zilizo kuwa zikitolewa na watumiaji wa mfumo wa Epicor iliyo tangulia
(Epicor 9.5) na kuzifanyia kazi kwa kutafuta suluhisho la changamoto hizo, na matokeo yake
ndio maboresho yanayo onekana katika Epicor 10.2 kwa hiyo Epicor 10.2 ni zao la watumiaji
wenyewe” amenukuliwa Masai.

Masai anasema chini ya Mradi wa PS3 ambao lengo lake mahsusi ni kushirikiana na kuzisaidia
halmashauri na serikali kwa ujumla katika kuongeza (kuboresha) urahisi na ufanisi wa utoaji
huduma kwa wananchi hasa walio pembezoni, kumekuwa na dhamira ya dhati katika
kuboresha mifumo mbalimbali ya kiutendaji ikiwemo Epicor na mifumo mingine iliyo katika
halmashauri zetu, ili kuongeza tija na uwajibikaji kwa wananchi wa Tanzania.

“Nadhani wote tunafahamu dhamira ya serikali ya awamu ya tano katika kufanya mageuzi
makubwa hususan katika utoaji wa huduma na uwajibikaji kwa wananchi, hatuwezi kuifikia
dhamira hiyo ya dhati kama hatuna mifumo imara na madhubuti kama huu wa Epicor 10.2 na
mingine mingi, ndio maana Shirika la USAID kupitia Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta ya
Umma (PS3) wamendelea kutoa ufadhili na ushirikiano wa kina katika kuimarisha mifumo
mbalimbali ya utoaji huduma kwa wanachi iliyo katika halmashauri nchini.

Jumla ya maofisa manunuzi 44 kutoka Halmashauri za Mikoa ya Kagera, Geita, Tabora, Mara,
Simiyu na wenyeji Mwanza wameshiriki mafunzo hayo ya mfumo wa Epicor 10.2,
yanayoendeshwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa Kushirikiana na Serikali ya Marekani kupitia
mradi wa kuimarisha mifumo ya Sekta ya umma PS3 kwa muda wa siku 2.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania