CURRENT NEWS

Monday, June 4, 2018

MAKADIRIO YA UJENZI WA CHUMBA CHA KUHIFADHIA MAITI MURRIET KUPITIWA UPYA  Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Josephat Kandege akitoa maelekezo leo wakati alipotembelea kituo cha afya cha Murriet kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kuona maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.


 Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Josephat Kandege akikagua  baadhi ya majengo yaliyojengwa katika Kituo cha afya cha Murriet kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kuona maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho


    Jengo la Kituo cha afya cha Murriet kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha , Jijini Arusha.


1 Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Josephat Kandege akikagua  baadhi ya mabati yaliyotumika katika ujenzi wa Kituo cha afya cha Murriet kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kuona maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho
.......................................................................................................
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Josephat Kandege amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe.Gabriel Fabian Daqorro kuhakikisha anaunda timu ya wataalam kuchunguza  ubora wa mabati yaliyotumika katika ujenzi wa kituo cha afya cha Murriet kilichopo katika kata ya  Murriet Halmashauri ya jiji la Arusha

Ameyasema hayo wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua ujenzi wa kituo cha Afya cha Murriet kuona maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kimepatiwa shilingi milioni 750 kwa ajili ya ujenzi wa wa majengo ya wodi ya Wazazi, Maabara, chumba cha upasuaji na chumba cha kuhifadhia maiti

Mhe Kandege amemtaka kuhakikisha anachunguza  gharama za ujenzi wa majengo hasa jengo la kuhifadhia maiti kwa kuwa gharama yake ni kubwa  ikilinganishwa na   ramani zilizotolewa na Serikali kwa nchi  nzima kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo.

Amemtaka Mkuu huyo wa Wilaya kuhakikisha wanafanya mapitio mapya ya makadiri ya ujenzi yaliyofanyika katika jengo la kuhifadhia Maiti ambapo gharama iliyokadiriwa ni shilingi milioni 51. Kwa jengo hilo.

“Sijaridhishwa na makadirio ya ujenzi yaliyofanyika katika jengo la kuhifadhia maiti kwa kuwa ramani hizo zimetolewa na Serikali nchi nzima kwa ajili ya ujenzi huo, hivyo namtaka Mkuu wa Wilaya kufanya mapitio mapya ya makadirio ya ujenzi wa jengo hilo.

Amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya nchini hivyo inahitaji kuona thamani ya majengo yanayojengwa yanaenda sambamba na fedha zilizotolewa na Serikali.

Mhe. Kandege ameziagiza Halmashauri zote nchini kubana matumizi ili kiasi cha fedha kitakachotolewa na Serikali kitumike kuongeza majengo mengine na kuimarisha yaliyopo ili kuweza kutoa huduma bora za afya kwa jamii.

Ameelekeza chumba cha kujifungulia akina mama wajawazito kitenganishwe kila kitanda ili kuwa na usiri mama mjamzito anapojifungua.

Aidha Mhe. Kandege ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Arusha kuhakikisha Ujenzi wa vituo vya afya unakamilika kwa wakati ili wananchi wapate huduma za afya karibu na maeneo wanavyoishi.

Wakati huohuo Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Bw. Athumani Kihamia amesema  jumla ya shilingi milioni 700 zimepokelewa  kwa ajili ya  umaliziaji wa jengo la OPD pamoja na  kujenga majengo ya wodi ya wazazi, Maabara, chumba cha upasuaji na chumba cha kuifadhia maiti ambapo zaidi ya shilingi milioni 462 zimetumika.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania