CURRENT NEWS

Tuesday, June 5, 2018

MFUMO WA UHASIBU KUONGEZA UWAZI NA UWAJIBIKAJI KATIKA HALMASHAURI

 Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia TEHAMA kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI bwana
Baltazar Kibola, akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya Mfumo wa Epicor
toleo la 10.2 kwa Wahasibu na WawekaHazina kutoka Mikoa ya
Morogoro, Iringa na Halmashauri za Jiji la Tanga, Muheza na Korogwe.
Washiriki wa  mafunzo ya Mfumo wa Epicor
toleo la 10.2 kwa Wahasibu na WawekaHazina kutoka Mikoa ya
Morogoro, Iringa na Halmashauri za Jiji la Tanga, Muheza na Korogwe.
Washiriki wa  mafunzo ya Mfumo wa Epicor
toleo la 10.2 kwa Wahasibu na WawekaHazina kutoka Mikoa ya
Morogoro, Iringa na Halmashauri za Jiji la Tanga, Muheza na Korogwe.

.............................................................................
Na Mathew Kwembe

Serikali imesema kuwa maboresho iliyoyafanya kwa kushirikiana na
Mradi wa PS3 ya kuwa na mfumo mmoja wa uhasibu ujulikanao kama
Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Umma, (epicor) tolea la 10.2 ni
hatua kubwa katika utekelezaji wa dhana nzima ya uwazi, uwajibikaji na
utawala bora katika usimamizi wa Fedha za umma na kuboresha
huduma kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa jana mjini Iringa na Mkurugenzi Msaidizi
anayeshughulikia TEHAMA kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI bwana
Baltazar Kibola, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Mfumo wa Epicor
toleo la 10.2 kwa Wahasibu na WawekaHazina kutoka Mikoa ya
Morogoro, Iringa na Halmashauri za Jiji la Tanga, Muheza na Korogwe.

Bwana Kibola alifafanua kuwa kutokana na maboresho yaliyofanyika ya
kuwa na mfumo mmoja wa usimamizi wa fedha za umma sasa itakuwa
rahisi kwa viongozi wa serikali kuweza kufuatilia taarifa mbalimbali za
serikali katika halmashauri zote 185.

“Katika mfumo huu wa usimamizi wa fedha haitakuwa rahisi mtu
kubadilisha taarifa, na hii itaongeza uwazi, na uwajibikaji, na pia
itachochea kuboreshwa kwa huduma wazipatazo wananchi,” alieleza.

Bwana Kibola aliongeza kuwa mfumo wa Usimamizi wa Fedha za
Umma, (epicor) tolea la 10.2 utawezesha mifumo yote ya msingi ya
usimamizi wa fedha katika sekta za umma kuwasiliana na kushirikishana
katika suala la utoaji wa taarifa.

“Kupitia mafunzo ya Epicor toleo la 10.2 washiriki watajengewa uwezo
kujua namna mifumo ya PlanRep (Mipango na Bajeti), FFARS
(Usimamizi wa Fedha zinazopelekwa na Serikali moja kwa moja
kwenye vituo) na LGRCIS (Mfumo wa Ukusanyaji wa Mapato ya ndani
ya Halmashauri) zitakavyobadilishana taarifa kupitia mfumo wezeshi wa
Muungano Gateway,” alieleza.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo msaidizi, maboresho yaliyofikiwa
kwenye mfumo wa Epicor 10.2 yatasaidia katika suala zima la utoaji wa
taarifa hasa kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma pamoja na
kuunganisha taarifa hizo kwenye Hesabu za Halmashauri, pia utatoa
taarifa za utekelezaji za mipango na bajeti kwa kuzingatia matumizi ya
fedha yaliyofanyika.
Naye Mweka Hazina kutoka jiji la Tanga bwana Cornery Sima alieleza
kuwa mfumo wa Epicor toleo la 10.2 utasaidia kutatua changamoto za
kutoonana kwa mifumo hiyo, ambapo sasa mifumo minne ya uhasibu
imeunganishwa na kuwa kitu kimoja.
Aliongeza kuwa mbali na kuimarisha uwazi na uwajibikaji kwani sasa
taarifa zitakuwa zikionekana popote kwa kuwa mfumo wake utakuwa ni
mmoja.
Pia alisifu kuwepo kwa mifumo ya kihasibu kwani itapunguza matumizi
ya kutumia makaratasi, ambapo tofauti na kuandika hundi kwa njia ya
mkono, mfumo huu wa malipo umeunganishwa moja kwa moja na benki
kuu.
Mapema mgeni rasmi kwenye mafunzo hayo Katibu Tawala Mkoa wa
Iringa, Bibi Wamoja Ayubu alisema kuwa lengo la kuwajengea uwezo
ili muweze kusimamia mapato na matumizi ya Fedha za Umma kwenye
Halmashauri na pia kuwapatia uelewa wa mabadiliko ya msingi
yaliyofanyika bila kukwamisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aliongeza kuwa wao kama Makatibu Tawala wa Mikoa, ambao ni
viongozi wa Mikoa watahakikisha matumizi sahihi ya mifumo
yanakuwepo ikiwemo matumizi ya taarifa katika kufanya maamuzi
kuanzia ngazi za vituo vya kutoa huduma mpaka ngazi ya Mkoa.
Mafunzo hayo ya Mfumo wa Epicor toleo la 10.2 kwa Waweka Hazina,
Wahasibu, Maafisa Manunuzi, Maafisa TEHAMA pamoja na Maafisa
Usimamizi wa Fedha wa Mikoa yataendeshwa na wakufunzi kutoka
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),
wakishirikiana na wataalam kutoka mradi wa PS3.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania