CURRENT NEWS

Saturday, June 9, 2018

UMISSETA KUFANYIKA DODOMA MWAKANI


Na Mathew Kwembe, Mwanza
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa ametangaza kuwa mashindano ya michezo ya Umoja wa Michezo wa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) yatafanyika mkoani Dodoma.
Kwa miaka mitatu mfululizo mashindano hayo yamekuwa yakifanyika mkoani Mwanza katika viwanja vya chuo cha ualimu Butimba.
Akifungua rasmi mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA kwa mwaka huu katika uwanja wa CCM Kirumba jana Waziri Mkuu alisema kuwa pamoja na mkoa wa Mwanza kufanya maandalizi mazuri ya kuwapokea wanafunzi zaidi ya 6000 wa shule za msingi na sekondari mashindano hayo hayana budi kufanyika katika mkoa mwingine.
Waziri Mkuu alisema kuwa serikali inatambua na kuthamini sana mchango wa kuwepo kwa mashindano hayo katika kuibua vipaji vya wanafunzi katika michezo mbalimbali, hivyo akawataka wadau wa michezo nchini kuunga mkono juhudi hizo ili vipaji vya wanafunzi hao viweze kuendelezwa.
Mhe.Majaliwa aliwaasa wanamichezo wanaoshiriki mashindano hayo kutambua fursa zilizo mbele yao kwani michezo ina nafasi kubwa katika kutoa ajira.

“Chezeni kwa malengo, natambua uwepo wa viongozi wa vilabu vya Simba, Azam na hata Yanga wapo hapa, naamini wakiridhika na vipaji vyenu watawachukua na kuwalea katika kambi zao” alieleza.
Hata hivyo Waziri Mkuu aliwaagiza walimu na Maafisa Elimu waliopo katika timu hizo kuhakikisha kuwa hawatowaruhusu wasio wanafunzi kushiriki michezo hiyo.
“Tukigundua kuwa kuna mkoa una timu yenye wanafunzi mamluki hatua kazi zitachukuliwa dhidi yao,” alionya Waziri Mkuu.

Pamoja na kuwataka waheshimiwa madiwani kutenga bajeti ya kutosha kuendeleza michezo katika halmashauri zao aliwahimiza walimu kuhakikisha kuwa wanafundisha somo la haiba ya michezo shuleni.
Aliwakumbusha walimu kutumia vipindi vya michezo kufundisha michezo huku akisisitiza kuwa walimu wenye taaluma ya michezo ndiyo wapangiwe kufundisha vipindi hivyo na siyo vinginevyo.
“Michezo ifundishwe na wenye taaluma ya michezo msipeleke waelekezaji kufundisha michezo hiyo shuleni,” alisema.
Aliongeza kuwa hata kwenye mashindano haya anatarajia kuona kuwa washiriki ni walimu wa michezo badala ya kuleta walimu wasindikizaji.
Alisema kuwa tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli ameagiza kuwa michezo ichezwe tangu ngazi ya awali.

Kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kuzungumza, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia elimu Mhe. Joseph Kakunda alisema kuwa mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA yameliletea heshima kubwa taifa kwa kuibua vipaji vya wanamichezo mahiri.
Mhe.Kakunda aliwataja baadhi ya wanamichezo hao kuwa ni pamoja na Mbwana Samata, Edibily Lunyamila, Leodger Tenga na wengineo kwa umahiri wao mkubwa ambao chimbuko lake lilianzia katika mashindano haya.
Aliongeza kuwa mbali ya sekta ya michezo kuleta burudani katika taifa lakini imekuwa ni sekta muhimu kiuchumi huku akitolea mfano wa nchi ya Brazil ambayo kupitia sekta hiyo imeweza kuinua uchumi wake.
Pia Mhe.Kakunda alimuomba Waziri Mkuu kuhakikisha kuwa taifa linawekeza katika michezo kwa bajeti ya michezo kuboreshwa hasa katika ngazi za halmashauri.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Dkt Leonard Akwilapo ambaye alimwakilisha Waziri wake Profesa Joyce Ndalichako pamoja na kupongeza kuendelea kufanyika kwa michezo hiyo alisema kuwa wizara yake itaendelea kuboresha mitaala ya michecho mashuleni
Mapema Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Bwana Tixon Nzunda alisema kuwa katika mashindano ya mwaka huu jumla ya wanamichezo 3,360 kutoka mikoa 28 ikiwemo miwili kutoka Zanzibar wanashiriki kwenye UMISSETA ambapo michezo 10 itashindanishwa.

Kwa upande wa UMITASHUMTA alisema kuwa jumla ya wanamichezo 3120 kutoka mikoa 26 ya Tanzania bara watashiriki ikiwa ni wachezaji 120 kila mkoa.

Jumla ya michezo 9 ikiwemo mpira wa miguu wavulana na wasichana, mpira wa miguu maalum (wavulana viziwi), Netibali kwa wasichana, mpira wa wavu, mikono, kengele kwa wasioona, riadha maalum, riadha kawaida na sanaa za maonyesho.
Naye Naibu Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo Juliana Shonza pamoja na kumshukuru Waziri Mkuu kwa nasaha zake alisema kuwa wizara yake kwa kuwa ndiyo yenye dhamana ya michezo itaendelea kuisimamia sera ya michezo nchini.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania