CURRENT NEWS

Saturday, June 2, 2018

WAFUGAJI NCHINI WATAKIWA KUUNDA VYAMA VYA USHIRIKA Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Josephat Kandege akikagua moja ya machine inayotumika katika usindikaji wa maziwa kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya maziwa kilichofanyika leo katika viwanja Nanenane Themi, Mkoani Arusha.
 Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Josephat Kandege akikabidhiwa maziwa kwa ajili ya shule mbalimbali katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya maziwa kilichofanyika leo katika viwanja Nanenane Themi, Mkoani Arusha.
 Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Josephat Kandege akiwa na baadhi ya viongozi wakati akitembelea mabanda ya maonyesho kwenye  kilele cha maadhimisho ya wiki ya maziwa kilichofanyika leo katika viwanja Nanenane Themi, Mkoani Arusha.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Josephat Kandege akiongea na wadau wa ufugaji katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya maziwa kilichofanyika leo katika viwanja Nanenane Themi, Mkoani Arusha.
.............................................................
Angela Msimbira OR-TAMISEMI

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Josephat Kandege  amewaagiza wafugaji nchini kuunda  vyama vya ushirika imara ambavyo vitawezesha  kupata huduma za mifugo na kuboresha ukusanyaji na masoko ya maziwa. 

Mhe Kandege ameyasema hayo kwenye kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Maziwa iliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Nanenane, Themi Mkoani Arusha
Mhe. Kandege amesema uwepo wa ushirika imara utaboresha ukusanyaji wa  maziwa kwa wingi kwa ufanisi zaidi na hatimaye  kuongeza kiasi cha usindikaji kwa viwanda. 

“Napenda kutoa pongezi kwa wafugaji wa Mikoa ya Tanga na Njombe kwa kuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa mafanikio yanayoonekana katika kuendeleza tasnia ya maziwa kupitia ushirika” Amesema Kandege

Amesisistiza kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na idara zake nchini kuhakikisha zinawezesha uundwaji wa vyama vya ushirika imara na pia wanaimarisha vyama vya ushirika vilivyopo.

“Mtambue kuwa kuwepo kwa ushirika imara kunaweza kutatua changamoto nyingi. uwezo wa viwanda vya kusindika maziwa hapa nchini bado ni mdogo ukilinganisha na uwezo halisi wa viwanda hivyo”. Amesema Kandege

Mhe. Kandege ametoa rai kwa wadau wa sekta binafsi kujitokeza kwenye maonesho ya wafugaji kwa malengo ya kuongeza tija na kuimarisha viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo kwa kuwa  Serikali itaendelea kutoa msukumo wa pekee katika kuendeleza ufugaji wa kisasa nchini na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya tasnia ya maziwa wanaendelea kukamilisha mchakato wa  kuandaa mpango kabambe wa kuendeleza mifugo ambao unahusisha pia tasnia ya maziwa nchini.

Amewataka wadau wengine kuwekeza katika kujenga na kuendesha viwanda vya maziwa hapa nchini ili kuongeza uwezo wa kuzalisha zaidi bidhaa ambazo ni bora na zenye viwango vya kimataifa ili kukidhi mahitaji ya soko.

Kuhusu uhaba wa ng’ombe wa maziwa Mhe Kandege Serikali imeandaa mpango kabambe wa kuhakisha upatikanaji wa ngo’mbe bora wa maziwa kwa kuzalisha ndama milioni moja wa ng’ombe wa maziwa kila mwaka na  TAMISEMI na Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za uhimilishaji na upatikanaji wa gesi ya nitrojeni kwa kukiimarisha kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) na vituo vya Kanda na ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. 

Mhe. Kandege amesema Wafugaji wanapaswa kuboresha mbinu zao za uzalishaji kwa kuzingatia kanuni za ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa. Na muhimu zaidi wafugaji waunde vyama vya ushirika ambavyo vitaongeza tija katika upatikanaji wa pembejeo, huduma za ugani na huduma za kifedha. 

Amesema vyama ya ushirika vitakuwa kitovu cha upatikanaji wa huduma na masoko ya maziwa wanayozalisha. Wasindikaji pia waendelee kukusanya maziwa yanayozalishwa kutoka kwa wafugaji na kuyanunua kwa bei nzuri ili kutoa motisha kwa uzalishaji zaidi wa maziwa na kuyasindika.

Mhe Kadege  amewaagiza Mameya/ Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wote na wakuu wa Idara za Mifugo na Uvuvi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanahudhuria  bila kukosa katika maonesho yajayo ambayo Kimataifa yatafanyika Jijini Arusha ili waweze kujifunza  na kwenda kutoa elimu kwenye Halmashauri zao. 

Aidha Katika hatua nyingine Mhe. Kandege alishiriki zoezi la ugawaji  wa maziwa kutoka  kampuni ya Asas ya Iringa katika shule za msingi Terrati, Madosoita,Suye, Losiyo,Nkonoo, Osunyai na Kimandolo zilizoko Mkoani Arusha.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania